WANANCHI WAMUOMBA MBUNGE WAITARA KUINGILIA MGOGORO KATI YA WANANCHI WA KATA YA KWIHANCHA NA HIFADHI YA SERENGETI

Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na wananchi wa kata ya Kwihancha
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na wananchi wa kata ya Kwihancha
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mwita Waitara akizungumza na wananchi wa kata ya Kwihancha

**
Na Dinna Maningo,Tarime.

Wananchi wa kata ya Kwihancha wamemuomba Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mwita Waitara kuingilia kati mgogoro wa mpaka kati ya vijiji na hifadhi ya Serengeti ambao umesababisha baadhi ya watu kupoteza maisha.

Mbunge Waitara akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa amezungumza na wananchi wa kata ya Kwihancha ambapo Diwani wa kata hiyo Magita Mato amesema kuwa tangu mwaka 2015 watu 9 wameuliwa wakidaiwa kuingia ndani ya hifadhi na kwamba eneo la Tindiga ya Gong'ora,Kijito cha Sweto na mto Mara ni maeneo ambayo mifugo hukamatwa na watu kuuawa.

Diwani huyo aliwataja waliouawa kuwa ni Lucus Gasaya,Wambura Maisori,Goryo Ghati,Kebacho Wanko,Mwita Makuri,Nyagwisi Manga,Chacha Megoko,Wanene Masiaga na Chacha Nyaiho.

"Sisi tunatambua mpaka wa mwaka 1968 kati ya hifadhi na kata ya Kwihancha miaka ya nyuma tuliwahi kufanya uhakiki wa mipaka na watu wa hifadhi lakini kila mara wanazidi kuongeza,nusu ya eneo la tindiga liko kifadhini na nusu liko kwenye kijiji ambalo ndilo mifugo huchungia.

"Eneo hilo lina udongo wa chumvi chumvi,udongo huo hujenga mifupa ya wanyama na unatoa minyoo tumboni ni eneo linalopendwa na mifugo lakini TANAPA wamelichukua lote bado tena wameingia hadi mita 60 eneo la kijiji mifugo inateseka", alisema.

Rugura Wankaba alisema kuwa mpaka umeleta shida na migogoro mikubwa na kwamba maeneo yanayodaiwa kuwa ni hifadhi si kweli ni ya wananchi ambayo walikuwa wakilisha mifugo na kuishi tangu 1981 na sasa wamefukuzwa na hivyo kukosa maeneo ya kulima na malisho.

Msabi John alisema"Wakati wa uhakiki wa mipaka kati ya Tanzania na Kenya nilishiriki kwenye uwekaji wa Bikon,na GPS zilikuwa zinaonyesha mipaka lakini nashangaa hawatumii ramani za zamani zilizokuwa zinatambulika wao wamekuwa ni kuhamisha bikoni leo iko huku siku chache baadae unakuta zimesogezwa mbele".

Mwenyekiti wa kijiji cha Karakatonga Amos Waisahi alisema"Hivi karibuni baada ya mwananchi Chacha Megoko kuuwawa  tuliitwa tukaenda Nyamwaga kuhojiwa kuhusu mauwaji lakini hadi sasa hatujapewa majibu,na kuna watu wawili waliuwawa na Tembo ambao ni Mohoni Nyagichonge na Juma Mahara lakini hatujawahi kuona Serikali ikichangia chochote mazao yanaharibika hakuna utatuzi".

Mbunge wa jimbo hilo Mwita Waitara alisema kuwa atawasiliana na Waziri wa Maliasili na Waziri wa Ardhi kufika kusikiliza kero za wananchi na kuzunguka maeneo yote yanayopakana na hifadhi ili kupitia mipaka.

"Niliambiwa nyumba zimechomwa,mazao yamefekwa na ni nje ya hifadhi ,nikiongea na hifadhi nao wanasema nyumba na mazao yaliyochomwa yako ndani ya hifadhi,nitaongea na waziri ili nao wasikilize kero zenu tupitie mipaka na tuone chakufanya", alisema Waitara.

Naye Mtendaji wa Kata ya Kwihancha David Giriri alitaja changamoto za kata hiyo zikiwemo za upungufu wa walimu 38,nyumba za walimu 65,madarasa 46,vyoo matundu 114, madawati 551, meza 63,viti 56, ofisi 12 na watoa huduma ya afya 9.

Mbunge Waitara alimuagiza mtendaji huyo kuwakamata viongozi waliopita waliofuja fedha za vibanda vya soko sh. milioni nne ambapo naye alichangia sh. milioni tano katika ujenzi wa madarasa.

Mbunge huyo akiwa katika ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa aliongozana na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya na viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tarime akiwemo katibu wa CCM wilaya Hamis Mkaruka,Katibu Mwenezi,Mrema Sollo,Katibu wa Vijana Newton Mwongi na Katibu Hamasa Remmy Mkapa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments