MTU TAJIRI ZAIDI DUNIANI AANIKA SIRI 6 KUFANIKIWA KATIKA BIASHARA ZAKO..HIZI HAPA


Ni nini kinachompatia Elon Musk ufanisi katika biashara?

Siku chache zilizopita Elon Musk alitangazwa kuwa mtu tajiri zaidi duniani, akimpiku mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos.

Utajiri wa mfanyabiashara huyo wa magari ya Tesla na SpaceX umepita dola bilioni 185 sawa na euro 136 bilioni baada ya bei ya hisa za kampuni yake ya magari kupanda.

Lakini je ni nini siri ya ufanisi wake katika biashara? Miaka michache iliopita alizungumzia suala hilo kwa karibu saa moja alipohoijwa na BBC.

1. Cha msingi sio pesa

Kulingana na mtazamo wa biashara wa Elon Musk - cha msingi sio pesa.

Alipohojiwa mwaka 2014 alisema hajui kiwango cha utajiri wake.

"Sio kwamba kuna rundo la pesa zilizohifadhiwa mahali," alisema. "Ukweli ni kwamba nina hisa kadhaa katika Tesla, SpaceX, na SolarCity, na katika soko la hisa kila hosa niliyo nayo ina thamani yake ."
Aina ya gari ya Tesla X 90D ikiwa katika onyesho la kibiashara mjini Brussels.

Hapingi mbinu zozote za kutafuta mali "ikiwa inafanyika kwa kuzingatia maadili na njia nzuri", lakini anasema sio jambo linalompatia msukumo.

Mbinu hiyo bila shaka inonekana kufanya kazi.

Kampuni yake ya magari ya umeme Tesla, imefanya vyema baada ya thamani ya hisa zake kuongezeka hadi zaidi ya dola 700 bilioni katika miaka ya hivi karibuni.

Fedha hizo zinatosha kununua Ford, General Motors, BMW, Volkswagen na Fiat Chrysler, na bado asalie na fedha za kununua gari la Ferrari.
Robert Downey Jr anasema ametumia mbinu ya Musk katika aonyesho lake la Iron Man

Lakini Musk, ambaye anafikisha umri wa miaka 50 mwaka huu, hatarajii kufariki akiwa tajiri.

Anasema fedha zake zitatumika kujenga majumba katika sayari ya Mars na anasema hatoshangaa kuona utajiri wake wote ukimalizikia katika mradi huo.

Sawa na Bill Gates, huenda akachukulia kama ishara ya kufeli maishani akiwa atasalia na mabilioni kadhaa kwa sababu atakuwa hajatumia fedha hizo kwa njia nzuri.

2. Fuatilia ndoto zako

Ndoto ya kuwa na majumba katika sayari ya Mars ni kidokezo ambacho Elon Musk anaamini ndio ufunguo wa mafanikio.

"Unataka vitu vijavyo maishani kuwa vizuri," aliambia BBC. "Unataka vitu hivi vipya ambavyo vitafanya maisha kuwa bora."

Kwa mfano SpaceX. Alisema alibuni kampuni hiyo baada ya kuhisi kwamba mpango wa Marekani wa anga za mbali haukuwa na malengo ya juu zaidi.

"Nilitarajia kuona vitu vya hali ya juu zaidi ambavyo havipatikani duniani vikibuniwa, binadamu kuishi katika sayari ya Mars, kuwa na makao mwezini, na safari za ndege za mara kwa mara kwenda anga za mbali," alisema.

Wakati hilo halikufanyika, alizindua mpango wa "Mars Oasis Mission", ambao ulilenga kuanzisha kilimo cha kisasa cha kutumia nyumba katika sayari nyekundu.

Lengo lilikuwa kuwapa matumaini watu kuhusu masuala ya anga za mbali, na kuishawishi serikali ya Marekani kuongeza mgao wa bajeti ya Nasa.

Ni wakati alipokuwa anajaribu kuanzisha mradi huo ndiposa aligundua tatizo sio "kutokuwa na utashi, bali ni ukosefu wa njia" - teknolojia ya anga za mbali ni ghali zaidi kuliko jinsi inavyotakiwa kuwa.

Na kutokana na wazo hilo! Biashara ya bei rahisi zaidi ya utengenezaji roketi ilizaliwa.
Roketi ya SpaceX ikiandaliwa kufanya majaribio ya kwanza katika kiwanda cha kampuni hiyo mjini Boca Chica, Texas mwezi

Na cha kushangaza katika mradi huo ni kwamba haukubuniwa kwa lengo la kutengeza pesa, bali kumpeleka binadamu katika sayari ya Mars.

Musk alisema anajichukulia kama mhandisi kuliko mwekezaji, na kuongeza kuwa kile kinachomuamsha kila asubuhi ni kusuluhisha matatizo ya kiufundi.

Ni hilo ndilo limekuwa lengo lake la kwanza badala ya kuwa na dola kwenye benki na ametumia kanuni hiyo kama kigezo cha kujiendeleza maishani.

Anafahamu kila kizingiti anachovuka katika biashara yake kinamsaidia akiwa mtu anayejaribu kutafuta suluhisho la tatizo sawa na hilo - na kuendelea hivyo daima.

3. Usiogope kuwa na mawazo makubwa

Moja ya mambo makuu kuhusu biashara ya Elon Musk ni udhubutu wake.

Anataka kubadilisha kabisa kampuni ya magari, kuwa na koloni Mars, kutengeza treni za mwendo kasi kupitia bomba la hewa, kujumuisha AI katika ubongo wa binadamu kuimarisha nguvu ya jua na kampuni za betri.

Hii inamaanisha miradi yake yote inalenga siku za usoni sawa na vitu ambavyo ungesoma katika majarida ya watoto mapema miaka ya 1980.

Kwa mfano, biashara yake ya bomba inaitwa ''The Boring Company''.

Musk bila shaka hafanyi siri kuwa mawazo yake yalichangiwa na vitabu na filamu alizotazama akiwa mtoto nchini Afrika Kusini.
Kiwanda kipya cha Tesla kikijengwa mjini Shanghai, China mwaka 2019

Hatua hiyo inatupeleka katika kidokezo cha Musk cha tatu cha biashara - usijinyime.

Anaamini kuwa na malengo madogo ni changamoto kwa kampuni nyingi' hali ambayo inachangia miundo ya motisha.

Kampuni nyingi zinaangazia "kujiongeza", alisema. "Ukiwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni kubwa na malengo yako ni ya ukuaji wa kadri, itachukuwa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa, na matokeo yasiwe mazuri kama ilivyokusudiwa, basi hakuna atakaye kulaumu," aliambia BBC.

Unaweza kusema haikuwa kosa lako, ni kosa la wasambazaji.

4. Kuwa tayari kuchukua hatua ya hatari

Hii bila shaka ni jambo la kweli.

Lazima uwe mkakamavu kuchukua hatua hii, lakini Elon Musk amezidisha hatua hiyo kuliko wafanyabiashara wengi.

Kufikia mwaka 2002 alikuwa ameuza biashara zake mbili, muongozo wa jiji kupitia intaneti unaoitwa Zip2 na kampuni PayPal ambayo ni ya malipo mtandaoni.

Alikuwa ndio mwanzo ametimiza miaka 30 na tayari alikuwa na karibu dola milioni 200 kwenye benki.

Anasema mpango wake ulikuwa kuwekeza nusu ya utajiri wake kwenye biashara na kujiwekea nusu nyingine.

Mambo haykuwa hivyo alipokutana na mwandishi wa BBC, alikuwa ndio mwanzo anaibuka katika kipindi kibaya zaidi cha biashara maishani mwake.

Kampuni zake mpya zilikabiliwa na kila aina ya changamoto. Safari tatu za kwanza za roketi ya SpaceX zilitibuka, na Tesla ilikumbwa na kila aina ya matatizo ya uzalishaji, usambazaji na masuala ya muundo.
Vituo kadha wa kadha za kuchaji magari ya umeme zinabuniwa kati kati ya miji

Halafu mzozo wa kiuchumi ukaibuka.

Musk anasema alilazimika kufanya maamuzi magumu. "Ima aamuwe kuhifadhi pesa zake na kuacha kampuni zifilie mbali ama awekeze fedha zote alizosalia nazo kujaribu bahati yake ."

Aliendelea kumimina pesa.
Wakati mmoja alikuwa na madeni na kulazimika kuchukua mkopo kwa marafiki kujikimu kimaisha, aliambia BBC.

Je hofu ya kufilisika ilimtia uoga?

Anasema la hasha: "Watoto wangu huenda wakajiunga na shule za umma. Hiyo si hoja, hata mimi mwenyewe nilisomea shule ya serikali."

5. Puuza wakosoaji

Kilichomshangaza zaidi - na ambacho kilionekana wazi kumkera hata mwaka 2014 - ni jinsi wataalamu wengi na watoa maoni walivyoonekana kufurahia masibu yake.

"Ukosoaji ulikuwa wa kushangaza na hali ya juu sana," alisema Musk. "Blogu nyingi ziliangazia jinsi mradi wa Tesla unavyoelekea kuangamia."

BBC ilipendekeza kwamba watu walitaka mradi wake ufeli kwasababu alikuwa na kiburi.

Alipinga pendekezo hilo. "Nadhani ingelikuwa kiburi laiti tungelisema lazima tutafanikiwa, ukilinganisha na jinsi tulivyokuwa na hamu ya kufanikisha azma yetu na kujitolea kila tuwezavyo kufikia lengo hilo."

Hii inatupeleka katika kidokezo kingine cha ufanisi wa Musk katika biashara - usiwasikilize wakosoaji.

Aliambia BBC kuwa hakuwahi kuamini SpaceX au Tesla itawahi kurudisha kiwango cha fedha alichotumia karibuni - na ukweli ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyedhani hilo lingewezekana.

Lakini aliwapuuza wakosoaji na kuendelea mbele na mradi wake.

Kwa nini? Kumbuka huyo ni mtu ambaye anapima ufanisi wake kulingana na matatizo anayosuluhisha, na wala ni fedha kiasi gani anachopata.

Hii bila shaka ni kanuni ambayo inamweka huru. Hana hofu ya kuonekana mjinga kwa sababu fedha alizotumia hazikumnufaisha, kile anachoangazia ni umuhimu wa kufikia lengo.

Hali hii inafanya kazi kuwa rahisa kwasababu anaelekeza nguvu zote katika kitu ambacho anaamini kina umuhimu zaidi.

Na soko linaonaoneka kuvutiwa na kile anachofanya.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Morgan Stanley ambayo ni benki ya uwekezaji ya Marekani ilikadiria thamani ya SpaceX kuwa dolabilioni 100 ($100bn).

Kampuni hiyo imeimarisha uchumi wa usafiri wa anga za mbali, lakini kile kitakachomfanya Musk kujivunia zaidi ni jinsi kampuni yake ilivyoimarisha nafasi ya Marekani katika mpango wa angaza mbali.

Mwaka jana roketi yake ya Crew Dragon iliwapeleka wanajimu wakimataifa katika kituo cha angani, katika mpango wa kwanza wa aina hiyo kutoka ardhi ya Marekani tangu safari hizo zilipositishwa mwaka 2011.

6. Furahia unachofanya

Fuata muongozo huu ukiambanisha na bahati kidogo bila shaka utapata utajiri na umaarufu. Na baada ya hapo utaanza kutoka katika ganda lako.

Elon Musk anafahamika kuwa mchapa kazi kupita kiasi - anajivunia kufanya kazi kwa takriban saa 120 - kwa wiki ili kufanikisha uzalishaji wa gari la Tesla Model 3 hadi lilipoingia barabarani - na tangu wakati huo anaonekana kufurahia anachofanya.

Mwaka 2018 ilijipata mashakani na wasimamizi wa Marekani wa masuala ya fedha alipoweka ujumbe kwenye Twitter kwamba anapanga kubinafsisha kampuni ya Tesla, na wakati janga la corona lilipoilazimuTesla kufunga kiwanda chake cha San Francisco, alipinga vikali marufuku ya kutotoka nje.

Alitaja hofu kuhusu virusi hivyo kuwa "ujinga" katika Twitter, na kuelezea amri ya kukaa nyumbani kama "kifungo cha lazima", akisema ''haifai'' na kwamba inakiuka haki ya kikatiba.

Alitaja hofu kuhusu virusi hivyo kuwa "ujinga" katika Twitter, na kuelezea amri ya kukaa nyumbani kama "kifungo cha lazima", akisema ''haifai'' na kwamba inakiuka haki ya kikatiba.

Msimu wa joto alitangaza mpango wa kuuza mali yake akisema "zinakurudisha nyuma".

Siku chache baadaye aliandika katika Twitter kwamba atamuita mwanawe wa kiume aliyezaliwa X Æ A-12 Musk.

Licha ya hayo mwenendo wake usiotabirika ukionekana kutoathiri biashara zake huku mfanyabiashara huyo akiendelea kuwa na ndoto kubwa kama zamani.

CHANZO - BBC SWAHILI


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments