TAKUKURU YAREJESHA NYUMBA ILIYOPORWA KINYEMELA BAADA YA MMILIKI WAKE KUSHINDWA KULIPA MKOPO WA SHILINGI LAKI TATU KAHAMA


Wananchi wakishuhudia Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akimkabidhi nyaraka za umiliki wa nyumba mtoto wa marehemu Rose Edward ambayo ilikuwa imeuzwa kinyemela.
Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akimkabidhi nyaraka za umiliki wa nyumba mtoto wa marehemu Rose Edward ambayo ilikuwa imeuzwa kinyemela.

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Kahama imerejeshea nyumba yake Edward Mpolosi mkazi wa Mtaa wa Nyihongo wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambayo ilikuwa imechukuliwa na Masero Nyamhanga mfanyabiashara wa mikopo umiza baada ya kushindwa kulipa mkopo wa shilingi laki tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Mkuu wa Takukuru wilaya ya Kahama Frank Masilamba katika hafla maalumu ya kuikabidhi nyumba hiyo kwa familia ya Mpolosi alisema kuwa utaratibu uliotumika kujimilikisha nyumba hiyo uliofanywa na Masero ulikuwa ni batili na haukuzingatia sheria.

“Marehemu Edward alichukua mkopo wa shilingi laki tatu lakini alipochelewesha kulipa deni hilo liliongezeka riba hadi kufikia shilingi milioni 10 na laki 5 ndipo alilazimika kuingia mkataba batili wa mauziano ya nyumba hiyo huku mkopeshaji akijua wazi kuwa alikuwa anatenda kosa,”alisema Masilamba.

Alifafanua kuwa watoto wa Edward walifika katika ofisi za Takukuru kutoa taarifa kuhusu baba yao kudhulumiwa nyumba iliyopo katika kitalu J 165 mtaa wa Nyihogo walianza uchunguzi na kubaini kuwa makubaliano ya mauziano ya nyumba hiyo yalikuwa ni batili.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha alisema kuwa serikali imeamua kuikabidhi nyumba hiyo watoto wa Marehemu Edward ambao ni Rose na George ili waendelee kuimiliki baada ya Masero kubainika hana uhalali wa mauziano ya nyumba hiyo maelekezo.

“Hatutawavumilia wafanyabiashara wanaotumia fedha zao kunyanyasa wananchi wanyonge kwa kuwakopesha mikopo umiza ambayo imekuwa ikiendelea kupoka haki za watu wengine, tutaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaobainika kutoa mikopo umiza bila kufuata sheria za nchi,”alisema Macha.

Naye Rose Edward ambaye alikabidhiwa nyumba hiyo aliishukuru taasisi hiyo kwa kufanikiwa kuwarejeshea nyumba yao ambayo ilikuwa imetwaliwa kinyemela na familia ya Masero, mgogoro ambao umewasumbua kwa muda mrefu bila ya kupata mafanikio kutokana na mkopeji huyo kudai kuwa aliuziwa nyumba hiyo na marehemu baba yao.

“Tunaipongeza serikali kwa kutusikiliza sisi wanyonye baada ya baba yetu kufariki tulianza kupokonywa mali zake ikiwemo nyumba,tumeishi maisha ya shida kutokana na mgogoro wa nyumba yetu ambayo leo tumeirejeshewa,”alisema Rose.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments