MKE AJIUA KISA MUME WAKE KATOKA JELA


Jesca Samson (37) mkazi wa mtaa wa Katoma, Kayanga wilayani Karagwe anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu ya panya baada ya kusikia mume wake aliyefungwa kutokana na ugomvi wao ameachiwa kutoka jela.

Mwanamke huyo, kabla ya kifo chake anadaiwa pia alimnywesha sumu hiyo mtoto wake, Jordan Samson (3), ambaye hata hivyo alinusurika kifo.

Kamanda wa Polisi wa Mkao wa Kagera, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea Januari Mosi saa 8:00 usiku baada ya mama huyo kutoka katika mkesha wa Mwaka Mpya 2021.

Jesca, akiwa na ndugu zake, wakitoka kwenye mkesha, alipata taarifa kuwa mume wake ameachiwa huru na baada ya kusikia hivyo, aliwaacha njiani aliokuwa nao na kuwahi nyumbani kisha akanywa sumu hiyo.

Kamanda Malimi alisema baada ya ndugu zake kufika nyumbani, Jesca aliwaambia kuwa amekunywa sumu ya panya, ndipo walimpeleka hospitali ya Wilaya Nyakahanga pamoja na mtoto wake, na mwanamke huyo alifariki dunia Januari 2, huku mtoto wake akipona.

Mumewe ambaye hakutajwa jina, alikuwa amefungwa kifungo cha miezi mitatu jela kutokana na mgogoro wa kifamilia.

“Mgogoro uliokuwapo kati yake na mumewe ulitokana na mwanaume huyo kuuza kipande cha ardhi bila kumshirikisha mkewe na mwanamke akamshtaki katika mahakama ya mwanzo. Mume alihukumiwa kwenda jela miezi mitatu,” alisema Malimi

Alisema baada ya kusikia mme wake ameachiwa kutoka gerezani Desemba 31, 2020 alijenga hofu na hivyo kuchukua hatua za kunywa sumu ya panya na kunywesha mtoto wake.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Nyakahanga kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post