VIGOGO YANGA SC WAENDELEZA WIMBI LA USHINDI... WAICHAPA DODOMA JIJI FC 3 -1


VIGOGO, Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji FC jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi. 

Dodoma Jiji FC yenyewe iliyopanda Ligi Kuu msimu huu inabaki na pointi zake 19 baada ya kucheza mechi 14 katika nafasi ya 11.

Dodoma Jiji FC inayofundishwa na kipa wa zamani wa Yanga SC, Mbwana Makatta ilitangulia kwa bao la mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Seif Abdallah Karihe dakika ya tatu tu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Metacha Boniphace Mnata kufuatia krosi ya Dickson Ambundo kutoka upande wa kushoto.

Nahodha na beki Mghana, Lamine Moro akaisawazishia Yanga SC dakika ya 25 baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na Deus Kaseke na kugeuka haraka kumtungua kipa Aaron Kalambo.

Kipindi cha pili kocha wa Yanga SC, Cedric Kaze alikianza kwa kumuingiza mchezaji mpya, Mrundi mwenzake, Said Ntibanzonkiza ambaye alikwenda kuiongezea kasi safu ya ushambuliaji na kupata mabao mawili zaidi.

Ntibanzonkiza mwenyewe akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 69 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20 na ushei kufuatia yeye mwenyewe kuangushwa na kiungo Salmin Hoza nje kidogo ya boksi.

Beki mwingine wa kati, Bakari Nondo Mwamnyeto akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 75 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ntibanzonkiza kutoka upande wa kulia kufutia beki KIbwana Shomari kuangushwa na Ambundo.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mtibwa Sugar imeichapa 1-0 JKT Tanzania bao pekee la Riphat Msuya dakika ya 43 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Ihefu imeichapa 1-0 KMC bao pekee la Joseph Kinyozi dakika ya tisa Uwanja wa Highland Estates, Mbarali mkoani Mbeya.

Nayo Gwambina imelazimishwa sare ya 1-1 na Tanznaia Prisons Uwanja wa Gwambina, Misungwi, wenyeji wakitangulia kwa bao la Paul Nonga dakika ya kwanza, kabla ya wageni kusawazisha dakika ya 81 kupitia kwa Marco Mhilu. Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwanyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong/Said Ntibanzonkiza dk46, Deus Kaseke na Yacouba Sogne/ Ditram Nchimbi dk89.

Dodoma Jiji FC; Aaron Kalambo, George Wawa, Jukumu Kibanda, Justin Omary, Mbwana Bakari ‘Kibacha’/ Rajab Seif dk73, Salmin Hoza, Dickson Ambundo, Steven Silvester/ Cleiphace Mkandala dk84, Seif Karihe, Khamis Mcha na Peter Mapunda.

 CHANZO- BINZUBEIRY BLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post