WAZIRI MKUU ACHUKIZWA NA BANDARI YA KAGUNGA KUTOFANYA KAZI, ATOA WIKI MBILI KWA TPA

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipa wiki mbili kuanzia jana (Ijumaa, Desemba 18, 2020) Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ihakikishe kwamba ifikapo Januari Mosi mwakani Bandari ya kimkakati ya Kagunga iliyoko katika Kata ya Kagunga wilayani Kigoma iwe imeanza kutoa huduma.

“Leo nimekuja hapa kuona bandari, hii bandari ilikamilika mwaka 2017 imekaa tu, nyumba zimejaa popo tu na mle ndani kumejaa takataka na mmefagia jana baada ya kusikia mimi nakuja, hovyo kabisa nawauliza hapa wanajikanyaga tu tuna mtumishi hapa hakuna mtumishi amekuja jana badaa ya kusikia nakuja hovyo kabisa hawa.”

Alitoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Desemba 18, 2020) baada ya kukagua mradi wa bandari ya Kagunga iliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, wilayani Kigoma. Waziri Mkuu amechukizwa na kitendo cha bandari hiyo kushindwa kutoa huduma licha ya kuwa imekamilika.

Waziri Mkuu alisema mbali na bandari hiyo ya Kagunga kuanza kazi Januari Mosi, 2021, pia ameagiza soko la kisasa la Kagunga nalo lianze kazi siku hiyohiyo ili kuwawezesha wananchi wa Kagunga waanze kufanya biashara na kuinua kipato chao.

Pia, Waziri Mkuu alishangwaza na kuchukizwa na kitendo cha Meneja wa Bandari kutoka Makao Makuu ya TPA ambaye hajawahi kufika katika bandari hiyo na haijui. “Kama kweli wewe ni Meneja wa Bandari Tanzania bandari zako huzijui na unamiaka chungunzima unafanya kazi gani, hovyo kabisa.”

Waziri Mkuu alisema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo ulikamilika 2017 ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na la mizigo, nyumba ya kuishi mtumishi na jengo maalumu lakini hakuna mtumishi katika bandari hiyo ambayo ujenzi wake uligharimu shilingi bilioni 3.8.

“…Tarehe moja ya mwezi wa kwanza mwaka 2021 nataka bandari hii ianze kazi, nenda mkajipange. Hapa hakuna mtumishi hamisha watumishi kama wapo Dar es Salaam, kama wapo Kigoma leta watumishi hapa wawatumikie wananchi kwenye bandari hii.”

Aliwaagiza watendaji wa TPA waruhusu meli na boti za watu binafsi zifanyekazi ya kutoa huduma katika bandari hiyo ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo kwa urahisi. Amesema Serikali inataka majengo hayo yatumike kama ilivyokusudiwa. “Hizi fedha za Watanzania shilingi bilioni 3.8 watu wanafanya nazo mchezo tu, nataka nione bandari hii inafanya kazi.”

Pia, Waziri Mkuu aliwataka raia wa Burundi wanaohitaji kuingia nchini wahakikishe wanafuata taratibu zote za uhamiaji kabla ya kuingia nchini. “Sisi Tanzania na Burundi ni ndugu, ili kudumisha amani na kuimarisha ujirani mwema kila mmoja afuate sheria na taratibu zilizopo.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma, Pendo Mangali ahakikishe anashughulikia madai ya vijana waliokuwa wanafanyakazi za vibarua katika ujenzi wa miradi hiyo ya maendeleo wanalipwa stahiki zao. “Mkurugenzi hapa lazima uje tena, kajipange Jumatatu tarehe 21 Desemba, 2020 uje hapa ukutane na walalamikaji wote uratibu vizuri ili hawa wapate haki zao na Mheshimiwa Mkuu wa wilaya simamia hawa vijana wapate stahili yao.”

Waziri Mkuu yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments