TANZANIA, PAKISTAN ZASAINI MIKATABA YA MAKUBALIANO YA KIDIPLOMASIA


 Tanzania na Pakistan zimetiliana saini mikataba miwili ya makubaliano ambayo ni mkataba wa mashaurino ya kidiplomasia pamoja na mkataba wa kuanzisha tume ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi.

Mikataba hiyo imesainiwa jana Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi pamoja na Balozi wa Pakistani hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa makubaliano hayo yanatoa fursa nyingi zilizopo za kuongeza na kukuza biashara kati ya Tanzania na Pakistan hasa katika sekta ya kilimo ikiwemo chai, pamba, korosho, mbegu za mafuta, Madini ya Tanzanite, pamoja na uwekezaji.

“Tanzania na Pakistan zina uhusiano wa muda mrefu na katika mazungumzo yetu ya leo, Balozi wa Pakistan ameeleza fursa zilizopo Pakistan ambapo fursa hizo zikitumiwa vizuri zitanufaisha mataifa yote mawili,” Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa makubaliano hayo ni kielelezo kingine cha uhusiano mzuri uliopo baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Pakistan na kwamba fursa hizo zitaendelea kuongeze ushirikiano wa diplomasia ya uchumi baina ya Tanzania na Pakistan.

Kwa Upande wake Balozi wa Pakistani hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem amesema kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo muhimu itasaidia kukuza na kuendeleza diplomasia ya Uchumi baina ya Tanzania na Pakistan.

“Ni imani yangu kuwa kusainiwa kwa mikataba hii miwili ya makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Pakistan kutasaidia kudumisha na kukuza uchumi kati ya mataifa yetu,” Amesema Balozi Saleem


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments