NMB TARIME YAVIASA VIKUNDI VINAVYOKOPESHANA KUWA NA MIRADI, YAIPONGEZA SITAWISHA KUVUNA MILIONI 51.5

Na Dinna Maningo,Tarime

Afisa kutoka Benki ya NMB  Tawi la Tarime Kelvin Kaema amesema kuwa ili vikundi vipige hatua kiuchumi havina budi kuanzisha miradi mingi ambayo itawawezesha ku anasema kuwa kikundi hicho kinajiendesha kupata fedha badala ya kuishia kuchangishana na kukopeshana.

Kaema aliyasema hayo wakati akizungumza na wanakikundi cha Sitawisha kilichokuwa kikivunja mzunguko wa awamu ya pili ya kuchangishana fedha na kukopeshana ambapo walihudhuria watu mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vikundi,Idara ya Maendeleo ya jamii,Wenyeviti wa mitaa na Mchungaji wa kanisa la TPC Tarime.

Kaema alisema kuwa kikundi cha Sitawisha mbali na kuchangishana fedha kina mradi wa upishi na mradi wa biashara ya mazao ambayo itawaongezea fedha na hivyo kujiinua kiuchumi.

Alikipongeza kikundi hicho kwa ushirikiano na kwamba hakujatokea malalamiko yoyote ya kifedha na kupitia kikundi hicho na Benki imepata wanachama wengi wa kikundi ambao wamefungua akaunti zao na akaunti ya kikundi.

"Ni kikundi kinachojiendesha vizuri kinatunza fedha kwenye Benki yetu na wakitaka kukopesha fedha zao zinatumwa kwenye akaunti zao hawachukui mikononi maana watu wakivunja mizunguko usalama wa fedha ni mdogo unaweza kuvamiwa njiani ukatolewa fedha zako.

"Akaunti za vikundi hazina makato yoyote hata kama unaangalia salio au unatoa fedha kama kuna kikundi akaunti yao inakatwa fedha naomba waandike barua ya kubadilishiwa akaunti ", alisema Kaema.

Sospeter Samson ni miongoni mwa wanakikundi cha Sitawisha aliiomba Benki ya NMB kuvikopesha fedha vikundi kama njia ya kuvisaidia vikundi.

Kaema alisema suala la mikopo kwa vikundi lipo kwenye zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar- es- salaam na Morogoro na kuwaomba waendelee kuwa  wavumilivu huku akiwataka kuendeleza nidhamu.

Katibu mkuu wa kikundi cha Sitawisha Chacha Sabega alisema kuwa kikundi kina watu 39 kilianzishwa 2016, kipo mtaa wa Msati kata ya Nyamisangura katika halmashauri ya mji Tarime,kinakutana kila alhamis ya kila wiki na kila mmoja uchanga hisa moja sh.3,000,sh 2,000 ya ada,2,000 ya maafa zitolewazo kila mwezi na sh.1,000 kila wiki kwa ajili ya uendeshaji.

Katibu huyo anasema kuwa wamefanikiwa kukopesha fedha sh. milioni 51.5 kwa wanakikundi zilizotolewa na wanakikundi,kuanzisha mradi wa upishi kwa kununua vifaa vya kutumia kwenye upishi kama sahani,sufuria,majiko,ndoo za maji,sinia,vikombe na vinginevyo,mradi huo umewapatia faida ya sh.laki 290,500,wamefanikiwa kununua mazao ya chakula kwa zaidi ya milioni 12 ambayo wameyahifadhi kusubiri bei itakayowapa faida.

"Tunajivunia kupokea wanachama wapya 12 ambao ni ndani ya mzunguko huu wa pili,mzunguko uliopita tulivunja nzunguko tukiwa na wanachama 30 tukaanza mzunguko tukiwa na wanachama 29 sasa tumevunja mzunguko tukiwa na wanachama 39", alisema Sabega.

Aliongeza kuwa kuongezeka kwa wanachama kumesaidia ongezeko la uzalishaji wa rasilimali fedha za kikundi na za wanachama kupitia vyanzo vyake vya mapato ndani ya kikundi na wamefanikiwa kushiriki katika shughuli za kijamii kwa kuchangia ujenzi wa shule ya msingi Bugosi kwa kutoa tripu moja ya mawe na mifuko miwili ya saruji.

Sabega alieleza kuwa mbali na mafanikio hayo kikundi kinakabiliwa na changamoto ya kutopata mkopo wa fedha kutoka Halmashauri ya mji Tarime inayotolewa na Serikali kwa ajili ya vijana na wanawake,Elimu ndogo ya ujasiliamali,wanachama wawili kutomaliza mzunguko na kujitoa kwenye kikundi kutokana na sababu za kinidhamu.

"Kikundi kinatarajia kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga ofisi ya kikundi na sehemu ya kufanyia vikao vya kikundi,Kuinuana kielimu na kiuchumi miongoni mwetu kwa kuwaleta watu wa SIDO na waelimishaji wengine wa mambo ya ujasiliamali ili kuongeza tija kwa kikundi na wanakikundi" alisema Sabega.

Mchungaji wa kanisa la TPC Tarime Sostenes Magoma aliupongeza uongozi wa kikundi hicho na kukibariki kwa maombi.

"Kiongozi ni kila kitu,inapendeza ndugu wakikaa pamoja kwa umoja,watu wanaweza kukaa pamoja lakini si wamoja nawaombea mkae pamoja kwa umoja mtafanikiwa mambo yenu na mjitahidi kufuata taratibu za kikundi chenu",alisema Magoma.


Ghati Samwel Mratibu wa mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii(CHF) katika Idara ya Maendeleo ya jamii akampongeza Peter Mahiri aliyebuni wazo la kuanzisha kikundi hicho hadi sasa wameweza kukopeshana fedha nyingi.

Aliongeza kuwa hadi sasa kuna vikundi 546 na aliwaomba wanakikundi hao kujiunga na Bima ya afya ya jamii ambapo atatakiwa kulipa sh 30,000 itakayowezesha watu 6 katika familia yake kupata huduma ya afya.

Mwenyekiti wa kikundi cha Tavico John Magabe alisema kuwa awali vikundi vingi walijiunga wanawake pekee lakini kadri siku zinavyokwenda wanaume nao wamehamasika kujiunga kwenye vikundi vya kuchangishana fedha na kukopeshana baada ya kuona wanawake wamefanikiwa na anazidi kuwahamasisha wanaume kuendelea kujitokeza kujiunga na vikundi kwakuwa vinaleta mafanikio makubwa.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Julisu Chacha aliwataja baadhi ya wanakikundi ambao wameonyesha ushirikiano mzuri uliosababisha uongozi wa  kikundi kuwakabidhi vyeti ambao ni Chacha Sabega ambaye ni Katibu mkuu aliyekabishiwa cheti cha Uongozi bora,Mary Matias Cheti cha nidhamu,Thimoth Makondo mrejeshaji bora wa mikopo,Mwita Magabe mtunzaji bora wa rasilimali ya kikundi na Peter Mahiri mwasisi wa kikundi aliyeibua wazo la kuanzisha kikundi.

Peter Mahiri  alisema kuwa sababu ya kuanzisha kikundi hicho nikitokana na gharama kubwa  ya sh laki moja alizokuwa akiambiwa kutoa ndipo ajiunge na kikundi hivyo alitafuta watu wakafika wanne wakaanzisha kikundi kwa kuchangishana sh 5,000,kiliendelea kupata wanachama hadi wanavunja mzunguko wa kwanza walikuwa watu 30 wakiwa wamevuna milioni 22.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kenyambi Alphonce Shengoma alisema kuwa amekuwa akijiuliza nini sababu ya kikundi hicho kufanya vizuri na baada ya kushiriki hafla hiyo amegundua kuwa kikundi hicho kinafanikiwa kwakuwa kinamtanguliza mbele Mungu kwa maombi kwa kila jambo wanalofanya.
Afisa kutoka Benk ya NMB Tawi la Tarime Kelvin Kaema akizungumza na wanakikundi cha Sitawisha.
Julias Chacha Mwenyekiti wa kikundi cha Sitawisha akizungumza kwenye sherehe ya kuvunja mzunguko wa pili wa kikundi


Wanasitawisha wakiwa kwenye sherehe ya kuvunja mzunguko wa awamu ya pili
Mchungaji wa kanisa TPC akizungumza na kikundi cha Sitawisha
Katibu mkuu wa kikundi cha Sitawisha  Chacha Sabega
Wanasitawisha wakiwa kwenye sherehe ya kuvunja mzunguko wa awamu ya pili
Wanasitawisha wakiwa kwenye sherehe ya kuvunja mzunguko wa awamu ya pili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post