HALMASHAURI ZAAGIZWA KUJITATHMINI UKUSANYAJI WA MAPATO


Na. Angela Msimbira NJOMBE
Waziri wa Nchi Ofisi  ya  Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo  amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini  kujitathmini juu ya ukusanyaji wa mapato na usahihi wa utumiaji wa rasilimali fedha zitokanazo na mapato hayo

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo jana wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na kusema kuwa lazima mapato hayo yanayokusanywa yatumike kwa usahihi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo

“Nataka Halmashauri zote zikusanye mapato, awali ukusanyaji wa mapato ulikuwa hafukii asilimia 72, katika kipindi cha miaka mitano Chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli Halmashauri zote nchini zimeweza kukusanya mapato kwa asilimia 94” amesema Waziri Jafo

Waziri Jafo amesisitiza kuwa Serikali ilijiwekea mkakati kuwa   ifikapo  Disemba 2020  halmashauri  zote ziwe zimekusanya mapato si chini ya asilimia 50 , suala la ukusanyaji wa mapato ni la muhimu katika Halmashauri zote nchini.

“Nitakapotoa  ripoti ya  miezi sita ya  hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zote nchini mnamo tarehe 15/1/2020 nataka halmashauri zote  ziwe zimefikia si chini ya asilimia 50 ” amesisitiza Waziri Jafo

Amesema kuwa Halmashauri zote ambazo hazitafikia asilimi 50 ya ukusanyaji wa mapato Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  lazima ajitathmini kama anafaa kuendelea kushika nafasi au hatoshi na atolewe ili awekwe mwingine ambaye  atakayeweza kukusanya mapato

Waziri Jafo amesema Serikali haitashughulika na Wakurugenzi pekee bali itawachukulia hatua waweka hazina na maafisa mipango wa Halmashauri  ambao wameshindwa kukusanya mapato.

Aidha Waziri  Jafo  ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya  Njombe  ambapo walijiwekea malengo ya kukusanya  kiasi cha shilingi bilioni 2.3  na hadi kufikia tarehe 21/12/2020  wameweza kukusanya kiasi cha shilingi 1.7 sawa na asilinia 72 wakati Halmashauri ya mwisho  kwa ukusanyaji wa mapato ni Halmashauri ya Wilaya ya Makete iliyokusanya kiasi cha shilingi milioni 599 sawa na asilimia 25

Wakati huohuo , Waziri Jafo amewaagiza watumishi wa  Mamlaka za Serikali za Mitaa wote nchini  kufanyakazi kwa ushirikiano na weledi katika kuwatumikia wananchi na kutoa huduma bora kwa jamii

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Katarina Revocati amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020  Halmashauri za Mikoa zilikisia  kukusanya jumla ya shilingi bilioni 13 kutoka nyazo nya ndani ambapo hadi kufikia juni,2020 halmashauri zilikusanya  shilingi bilioni 15.8 sawa na asilimia 121 ya lengo la makusanyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post