AGIZO LA WAZIRI MKUU KUHUSU BIDHAA ZINAZOINGIZWA NCHINI


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka zote za udhibiti zihakikishe kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa ajili maonesho mbalimbali zinakuwa na viwango vya kimataifa na pia bidhaa zisizo na viwango na bidhaa bandia hazipati nafasi ya kuingia kwenye soko la Tanzania.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa viwanda wazalishe bidhaa kwa wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mbalimbali nchini jambo ambalo litawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei shindani katika soko.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana (Ijumaa, Desemba 4, 2020) baada ya kufungua Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania katika Uwanja wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa wa Mwalimu J. K. Nyerere, Dar-Es-Salaam.  Kaulimbiu ya maeneo hayo ni ‘Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania.’

“Watanzania tuachane na fikra potofu kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili. Hebu sote tununue bidhaa zetu ili kukuza ajira na pato la mtu binafsi na Taifa kwa ujumla. Sisi Watanzania tunazalisha vitu bora na vyenye uhalisia.”

Amesema uwekezaji unaofanywa lazima uzingatie uendelevu, ubora na tija kulingana na viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa katika shughuli za uzalishaji ili kuhimili ushindani na hata kuweza kunufaika na fursa za masoko zinazoendelea kujitokeza. “Nina hakika tukijipanga tutaweza kuwa washindani mahiri na bidhaa zenu zitaingia na kuleta ushindani mkubwa kwenye soko.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka wawekezaji na wazalishaji wote nchini wafanye biashara halali, walipe kodi kikamilifu na wahakikishe wanatunza kumbukumbu vizuri ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi za biashara zinazofanyika ikiwemo na nchi jirani na kuweza kuandaa sera mahususi za kuwasaidia.

“Wizara ya Viwanda na Biashara hakikisheni wazalishaji wanatumia vizuri sheria za uasilia wa bidhaa ili kuweza kukidhi matakwa na kutumia fursa ya masoko ambayo Serikali yetu imesaini mikataba ya maridhiano hususani soko la Afrika Mashariki, SADC, AGOA na fursa nyingine za masoko ya pamoja.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe viwanda vilivyo katika mamlaka zao vinashiriki kuonesha bidhaa wanazozalisha ili bidhaa hizo ziweze kutafutiwa masoko katika nchi mbalimbali duniani zikwemo nchi za Ukanda wa EAC na SADC kwa lengo la kuongeza mauzo ya Tanzania nje ya nchi.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara za Fedha na Mipango na Viwanda na Biashara ziendelee na mikakati ya kisera na kikodi ya namna ya kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje na kuongeza ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani ili kukuza viwanda vya ndani mfano; bidhaa za mbao, mafuta ya kula na saruji.

“SIDO kwa kushirikiana na VETA wekeni kipaumbele cha kutoa mafunzo na kubuni nyenzo zinazoendana na mahitaji makubwa yaliyomo katika jamii ikiwemo katika eneo la kuchakata mazao kama korosho, chikichi, ufuta, alizeti na matumizi ya TEHAMA katika kuboresha uzalishaji mali, ufanisi, viwango na kutafuta masoko.”

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kufanya maboresho katika uratibu wa maonesho mbalimbali ya Viwanda na Biashara ili yafanyike kwa kuzingatia kanda za uzalishaji nchini badala ya nguvu kubwa kuelekezwa Dar Es Salaam na miji mikubwa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments