MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA SINGIDA SASA HADHARANINa Abby Nkungu, Singida

TABIA ya baadhi ya wazazi na walezi kumaliza kesi za ukatili wa kijinsia katika ngazi ya familia badala ya kuzifikisha kwenye vyombo vya sheria imeanza kupungua mkoani Singida; hali inayoonesha kuwa vita dhidi ya vitendo hivyo wanavyofanyiwa zaidi wanawake na watoto wa kike huenda ikafanikiwa.

Hayo yamebainika katika Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wakati askari wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-NET) walipotembelea Gereza la Wanawake mkoa wa Singida kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kutoa msaada sitahiki.

Katika taarifa yao, ilielezwa kuwa kumekuwepo na ongezeko la watu kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili wa jinsia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tofauti na huko nyuma.

Taarifa hiyo iliyosomwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike inaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Novemba mwaka mwaka huu, jumla ya matukio 875 ya ukatili wa kijinsia wa aina mbalimbali yaliripotiwa tofauti na matukio 829 tu yaliyoripotiwa kwa kipindi kama hicho mwaka jana. 

Hatua hii imeelezwa na wadau kuwa ni mafanikio makubwa tofauti na awali ambapo wazazi na walezi walitajwa kuwa ni kikwazo kikuu katika kutokomeza vitendo hivyo na kuimarisha suala la Usalama na Ulinzi wa mtoto mkoani Singida kutokana na kumaliza kindugu masuala hayo.

Awali, ilielezwa kuwa ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo, ubakaji, mimba za utotoni na ulawiti ni vigumu kumalizika mkoani Singida kutokana na baadhi ya makabila kuoana kindugu; hivyo wengi wao hupenda kusuluhisha na kumaliza kifamilia kesi za ukatili wa kijinsia, zikiwemo zile za makosa ya jinai, bila kuzipeleka kwenye vyombo vya sheria kwa lengo la kulinda heshima ya undugu wao.

Ofisa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la SPRF linalojishughulisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Singida, Mwedinuu Beleko anasema hii ni nyota njema dhidi ya ukatili wa kijinsia.

“Tunashukuru sana Vyombo vya habari kwa kusaidia katika vita hii kwani baada ya kuweka hadharani kuwa wazazi na walezi wanamaliza kesi za jinai kindugu suala ambalo ni kosa kisheria, sasa tunaona mwamko wa kuripoti polisi matukio hayo umeongezeka” alisema

Takwimu kutoka Shirika hilo zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai mwaka 2018 hadi Februari 2019, jumla ya matukio 56 ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, wakiwemo walio chini ya miaka minane, yaliripotiwa kutokea kwenye eneo la mradi Wilayani Ikungi. Matukio hayo ni pamoja na ubakaji, ulawiti, vipigo na mimba shuleni.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa licha ya matukio hayo kuwa ni makosa ya jinai, ni matukio matatu tu kati yake ndiyo yaliyofikishwa Mahakamani, 12 yalimalizwa kwa suluhu ngazi ya familia huku mengine yakiishia Serikali za vitongoji, Vijiji, Kata na Vituo vidogo vya Polisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post