WADAU WA ELIMU WAIOMBA SERIKALI KUWEKA UTARATIBU KUBAINI WENYE ULEMAVU


Meneja wa Mradi wa Action Aid, Karoli Kadege akisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa Wadau wa elimu mjini Chamwino
Mmoja wa Wadau akichangia kwenye jambo wakati wa majadiliano
Wadau wa elimu Chamwino wakiwa kwenye majadiliano ya vikundi
**

Na Abby Nkungu, Singida
SERIKALI imeombwa kuweka utaratibu wa kuwabaini watoto wenye ulemavu kuanzisha ngazi ya kitongoji ili waweze kuandikishwa shule na kupata haki yao ya msingi kama wengine, tofauti na hivi sasa ambapo baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwaficha majumbani kutokana na imani potofu.

Mwito huo ulitolewa kwa nyakati tofauti huko Chamwino Dodoma na Halmashauri ya wilaya ya Singida ambapo mashirika ya AFNET, MEDO na Action Aid yaliwaleta pamoja wadau wa elimu kujadili ripoti ya utafiti uliofanyika Januari mwaka jana juu ya suala la utoaji wa elimu unaozingatia usawa wa kijinsia na mahitaji maalum katika shule 20 za Mradi huo unaofikia tamati mwakani.

Mtafiti Kiongozi, Jacob Kateri alisema kuwa pamoja na mambo mengine; ikiwemo utoro wa wanafunzi, uwiano mkubwa wa walimu na uhaba wa matundu ya vyoo shuleni, lakini uandikishaji mdogo wa wanafunzi wenye ulemavu ni miongoni mwa changamoto kubwa zilizobainika.

Kateri alifafanua kuwa wakati takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa asilimia 0.5 ya watoto wanaoandikishwa shule ni wenye ulemavu sawa na Singida, lakini kwa halmashauri ya Wilaya ya Chamwino utafiti unaonesha kuwa walioandikishwa ni asilimia 0.34 ambayo ni chini ya wastani wa Kitaifa.

Hata hivyo, alisema kuwa katika kila shule 10 za utafiti kwa Singida na Chamwino, tano zina watoto wenye ulemavu licha ya kukabiliwa na changamoto ya miundombinu duni ya kujifunzia na kufundishia.

Wakichangia hoja hiyo, wadau walisema kuwa sababu kubwa inayochangia baadhi ya wazazi na walezi kutowaandikisha shule watoto wao wenye ulemavu ni imani potofu wakidhani kuwa ni mkosi katika familia hivyo hawasitahili kutoka nje na pia kupata aibu kwa jamii inayozunguka.

Walisema sababu nyingine ni miundombinu duni ya kujifunzia na kufundishia katika baadhi ya shule ambapo watoto wengine wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita tatu ili kufikia shule jirani ambayo haina walimu wenye taaluma ya kufundisha walemavu na hakuna vyoo maalum.

“Mzazi mmoja alituambia kuwa mtoto wake ana ulemavu wa viungo hawezi kutembea mpaka shuleni, lakini pia hana uwezo wa kumnunulia baiskeli na hana fedha za kumlipia nauli ya basi kila siku” alisema Mkurugenzi wa Shirika la CHANGONET - Dodoma, Elizabeth Msuya ambaye alikuwa akifuatilia suala la uandikishaji watoto wenye ulemavu katika halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

“Hebu fikiria kwa mtoto anayetambaa chini halafu akaenda kwenye shule isiyokuwa na vyoo maalum kwa walemavu inakuwaje? Au asiyesikia akaenda shule ambayo haina mwalimu wa elimu maalum, ndio maana baadhi ya wazazi na walezi wanakata tamaa”, alisema mdau mwingine Batron Mwidowe.

Walisema, njia pekee ni kwa Serikali kuweka utaratibu madhubuti wa kubaini watoto wenye ulemavu kuanzia ngazi ya Kitongoji na kuhakikisha kuwa wanaandikishwa kwenye shule maalum zenye mazingira rafiki kulingana na mahitaji yao ili waweze kusoma kama wengine.

Ofisa elimu Vifaa na Takwimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Nyemo Masimba alisema kuwa ili kufanikiwa, hatua hiyo lazima iende pamoja na kila mdau kutimiza vyema wajibu wake na kwamba elimu bure haina maana Serikali kutoa kila kitu kwani kilichofutwa ni ada tu.

Hivi sasa Serikali inatekeleza Sera ya elimu Jumuishi inayotaka watoto wenye mahitaji maalum na ulemavu wa aina mbalimbali kusoma pamoja na wenzao wa kawaida katika shule moja bila kubaguliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post