Wizara Ya Ardhi Yawashukia Wasioendeleza Viwanja Na Kulipia Kodi Ya Ardhi


 Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa rai kwa wamiliki wote wa ardhi walio na viwanja visivyoendelezwa na kulipiwa kodi ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipia viwanja vyao ndani ya siku kumi na nne baada ya kupokea ankara ya madai na wasipotekeleza watanyanganywa viwanja vyao na kupatiwa watu wengine.

Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Denis Masami wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mtaa wa Chidachi jijini Dodoma ikiwa ni Mkakati wa Wizara kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati.

Alisema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi zake za ardhi za mikoa imeanzisha utaratibu wa kuwatembelea wamiliki wa ardhi kila mwisho wa wiki kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi na kutoa elimu ili kuwawezesha wamiliki wa ardhi nchini kutekeleza jukumu hilo bila shuruti.

‘’Maeneo mengi nchini yana viwanja visivyoendelezwa na wakati huo wamiliki wake hawavilipii kodi ya pango la ardhi jambo linaikosesha mapato serikali, baada ya siku kumi na nne tutaanza utaratibu wa kuzitwaa, kuvinadi ili kufidia deni na kumilikishwa kwa watu wengine’’ alisema Masami.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema, Wizara ya Ardhi inatekeleza mkakati wake wa kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kushirikisha wataalamu wa sekta ya ardhi na Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika mikoa kwa kupita nyumba kwa nyumba na kuwapelekea wadaiwa Ankara za madai ya ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine yatokanayo na sekta ya ardhi ili waweze kulipa.

Akiwa eneo la Chidachi jijini Dodoma na timu yake, Masami alibaini maeneo kadhaa yasiyoendelezwa na wamiliki wake kudaiwa kodi ya pango la ardhi sambamba na ukubwa wa eneo la shule ya St Merys Dodoma kuonesha kuwa na ukubwa wa Square mita 900 wakati uhalisia ni hekta 3.5 jambo alilolieleza kuwa limeifanya shule hiyo kulipia kiasi kidogo cha kodi ya pango la ardhi.

Kwa upande wake Afisa Ardhi wa Jiji la Dodoma Ruta Rwechugura alisema, wakati wa zoezi la kuwafuatilia wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi walibaini kukiukwa kwa baadhi ya taratibu na wamiliki wa ardhi na kutolea mfano ubadilishaji matumizi ya umiliki sambamba na baadhi ya wananchi kuuziana viwanja bila kubadilisha jina.

Aliwataka wamiliki wote wa ardhi walionunua viwanja kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha wanabadilisha umiliki kwa kufika ofisi za ardhi katika halmashauri husika ili kuiweka ardhi yao salama na kuwasisitizia wamiliki kutobadili matumizi ya kiwanja vyao bila kufuata taratibu.

Hata hivyo, wakati wa zoezi la kuwafikia wadaiwa wa kodi ya ardhi mmoja wa wananchi aliyefikiwa na zoezi hilo Faustine Mwakalinga aliipongeza Wizara Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wake wa kuwafikia wamiliki wa ardhi kwa lengo la kutoa elimu na kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na kuuelezea kuwa utaratibu huo unapaswa kuigwa na watendaji wengine wa  serikali katika kudai kodi kwani ni utaratibu ulio rafiki na unamhamasisha mdaiwa kulipa badala ya kuogopa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments