Aliyekuwa ananunua mahindi kwa bei juu akamatwa

Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma limemkamata Mfanyabiashara wa mazao ya mahindi Christopha Njako (30) maarufu kwa jina la ‘bilionea wa Mkako’ Mkazi wa kijiji cha Mkako Wilayani Mbinga na kumfikisha mahakamani kwa makosa matatu ikiwemo kijipatia zaidi ya Sh. bilioni 1.3 kwa udanganyifu

Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma ACP Simon Maigwa amesema, mfanyabiashara huyo amekamatwa jana na amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma kujibu mashtaka matatu yanayomkabili.

Inadaiwa kuwa, kuanzia Agosti mwaka huu mfanyabiashara huyo amekuwa akinunua mahindi kwa bei ya juu ya shilingi 75,000 kwa gunia moja na kuyauza kwa bei ya chini shilingi 45000 kitendo kilichowavutia wakulima wengi pamoja na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini ambao walifika katika kijiji cha Mkako kwa lengo la kuyauza mahindi yao na wengine kuyanunua mahindi na kuyapeleka kuyauza Mikoa ya Kaskazini na nje ya Nchi.

Ameeleza kuwa, ilipofika mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, biashara hiyo ilianza kuleta dosari, mashaka na taharuki kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara waliokuwa wamepeleka mahindi yao kuyauza kwa mfanyabishara Njako na ndipo malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wakulima ambao walimlalamikia Njako kushindwa kuwalipa fedha walizo peleka kuyauza mahindi yao na wengine walilalamika kuwa walimpatia fedha ili awapatie mahindi bila mafanikio.

Kamanda Maigwa amesema, baada ya kupokea na kubaini malalmiko hayo, Jeshi la Polisi lilichukua hatua stahiki ambazo ni pamoja na kufanya uchunguzi wa kina na kuupata ukweli kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akifanya biashara kwa njia ya ujanja na kuwatapeli wakulima na wafanya biashara zaidi ya 1200 ambao wanadai fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.3.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, amekuwa akitumia fedha hizo kuanzisha miradi mingine binafsi ambapo amejenga ghala la kuhifadhia mahindi, amejenga nyumba ya kulala wageni, amejenga nyumba ya kuishi na amenunua magari ya kifahari.

Baada ya Jeshi la Polisi kujiridhisha mfanyabiashara huyo amewatapeli idadi kubwa ya wananchi na kusababisha taharuki, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa ilichukuliwa hatua ya kumfikisha mahakamani mshtakiwa kwa makosa matatu na taarifa za ndani zimeonesha kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akifanya matendo hayo ya utapeli akishirikiana na jamaa zake wa karibu na upelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.

 

Credit: Majira



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments