BOSI WA JAMII FORUMS MAXENCE MELO AHUKUMIWA


Mkurugenzi mtendaji wa Jamii Forums, Maxence Melo
***
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mkurugenzi mtendaji wa Jamii Forums, Maxence Melo kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kutokufanya kosa lolote la kijinai baada ya kupatikana na hatia ya kuzuia askari kutekeleza majukumu yao.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumannne 17 Novemba 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam Huruma Shaidi baada ya kumkuta na hatia katika shitaka lake la kuzuia upelelezi wa Jeshi la Polisi.

Wakati akitoa hukumu ya kesi hiyo namba 458 ya mwaka 2016, iliyokuwa inamkabili Melo na mwenzake Mike Mushi, Huruma Shaidi amesema mahakama imemuachia huru Melo kwa masharti ya kutofanya kosa kama hilo ndani ya mwaka mmoja ambapo Mushi hakukutwa na hatia yoyote.

Katika kesi hiyo, Melo na Mushi walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili, kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa kwa kikoa cha Tanzania (.Tz) na kuzuia upelelezi wa Jeshi la Polisi.

Ambapo, Melo alikutwa na hatia katika shitaka la kuzuia Upelelezi wa Jeshi la Polisi huku mwenzake akikutwa hana hatia katika mashtaka yote mawili.

Katika kesi hiyo, Melo alikuwa akituhumiwa kutotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu wanachama wawili wa Jamii Forums waliodaiwa kuandika madai ya uhalifu uliotuhumiwa kufanywa na benki ya CRDB kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Chanzo - Mwanahalisi Online & Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments