WATEJA ZAIDI YA 1,000 WAJISHINDIA ZAWADI KAMPENI YA JIPE TANO YA BENKI YA CRDB

 

Dar es Salaam 5 Novemba, 2020 - Benki ya CRDB leo imetangaza washindi zaidi ya 1,000 ambao wamejishindia fedha kupitia kampeni yake ya ‘Jipe Tano’ ambayo ina lengo la kuwahamasisha wateja wake na umma wa watanzania kujenga utamaduni wa kuweka akiba itakayowasaidia kufikia malengo yao katika maisha na kujiimarisha kiuchumi yaliyo.

Akizungumza kuhusiana na washindi hao Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili alisema kila siku jumla ya washindi 240 wanapatikana kwa kuangalia wateja wanaoweka akiba katika matawi yote ya benki hiyo nchi nzima. Adili amesema zawadi hizo za fedha huingizwa moja kwa moja katika akaunti za wateja na hivyo kuendelea kumuhamasisha zaidi kuendelea kuweka akiba.

“… mteja anapoweka akiba kwenye akaunti yake iwe ni katika moja ya matawi yetu, kwa CRDB Wakala au kwa kuhamisha kutoka akaunti moja kwenda nyengine kupitia mitandao ya simu au kwa kuhamisha kutoka benki nyengine na akaunti za mitandao ya simu, anapata nafasi ya kujishindia zawadi,” anasema Adili.

Kampeni hiyo ya ‘Jipe Tano’ inatoa fursa kwa wateja kujishindia zawadi ya shilingi elfu tano kila wanapoweka akiba katika akaunti zao ikiwamo akaunti ya Watoto Junior Jumbo, Akaunti ya Malkia kwa ajili ya wanawake, Akaunti ya Scholar, Akaunti ya Vikundi ya Niamoja, pamoja na huduma nyengine za uwekaji akiba.

Akitoa pongezi kwa washindi wa kampeni hiyo ya ‘Jipe Tano’, Adili amewataka wateja wa Benki ya CRDB kushiriki kwawingi na kwamba wana nafasi kubwa ya kujishindia zawadi huku wakijahakikishia kuwa na akiba ya kutosha kwenye akaunti zao kwa ajili ya matumizi yao ya siku za usoni.

Adili alitumie fursa hiyo pia kuwahamasisha wazazi na walezi kuwafungulia watoto akaunti ya Junior Jumbo na kuanza kuwawekea akiba kidogo kidogo kwa ajili ya elimu na mahitaji mengine ya watoto. “… tunaelekea mwishoni mwa mwaka lakini pia hiki ndio kipindi cha kuanza kuweka akiba kwa watoto kwa ajili ya ada za shule, ili itakapofika januari tusisumbuke na suala la ada,” ameongezea Adili.

Akaunti ya Junior Jumbo ni akaunti maalum kwa ajili ya watoto inayomuwezesha mzazi au mlezi kutimiza malengo aliyojiwekea kwa mtoto hususan katika elimu. Mbali na kuwa akaunti hii haina gharama za uendeshaji, Adili alisema Akaunti hiyo hufunguliwa kwa kianzio cha akiba ya shilingi 20,000 na hutoa riba nono kwa amana za wateja. Mteja pia ana uhuru wa kuchagua aina ya sarafu ya kufungulia akaunti ikiwamo shilingi ya kitanzania, dola ya kimarekani, paundi ya uingereza.

“…. Katika kipindi hiki cha kampeni ya Jipe Tano, kila mzazi anapomuwekea akiba mtoto katika akaunti yake ya Junior Jumbo anapata nafasi ya kujipa tano na hivyo kuongeza akiba anayoweka wakati huo huo kutimiza malengo aliyojiwekea,” alisisitiza Adili.

Akaunti ya Junior Jumbo pia inasaidia kuwajengea watoto tabia ya kupenda kujiwekea akiba na hivyo kupata ufahamu juu ya elimu ya fedha.

--

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post