Rais Magufuli Apokea Gawio La Zaidi Ya Shilingi Bilioni 100 Kutoka Barrick


Na Beatrice Sanga & Lilian Shembilu-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amepokea gawio la zaidi ya shilingi bilioni 100 kutoka kampuni ya madini ya Twiga inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold Mining.

Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julisu Nyerere(JNICC), Jijini Dar es Salaam,  ampapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Barrick kwa kukubali kukaa chini na kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania yaliyopelekea kuanzishwa kwa kampuni ya Twiga Mineral Company ambayo imepelekea kuleta mafanikio kwa Watanzania ambao walikuwa hawafaidiki na madini wanayochimba.

“Napenda niwashukuru Barrick kwanza kwa kukubali kufanya mazungumzo na serikali, ninawashukuru sana kwa sababu mazungumzo yale yalichukua zaidi ya miaka miwili, wapo watu waliobeza sana na mpaka leo bado wapo na walikuwa ni Watanzania na ndio maana nasema Barrick ahsanteni sana” amesema Rais Magufuli

Ameongeza, kuwa  soko la madini nchini Tanzania limeongezeka kwa kiwango kikubwa  ambapo mwaka 2019 mapato yaliyokuwa yanatokana na madini yalikuwa hayazidi bilioni 268 lakini sasa mapato yanayotokana na madini yanafika bilioni 528.  Hii imetokana na jitihada mbalimbali ambazo serikali ya Awamu ya Tano imezifanya ili kuboresha  mifumo ya upatikanaji na uuzaji wa madini zikiwemo kuboresha  sheria ya madini ambayo imepelekea  wachimbaji wadogo na wakubwa kunufaika.

Rais Magufuli amebainisha kuwa sekta ya madini imetengeneza zaidi ya ajira milioni 1 kwa Watanzania lakini pia serikali ya Awamu ya Tano imeweza kutoa mafunzo kwa wachimbaji  zaidi ya 10,000  na kuimarisha taasisi ya geology nchini  ambapo imepelekea kukua kwa sekta ya madini.

Aidha Rais Magufuli  ametoa wito kwa Watanzania  na wasio Watanzania, wakiwemo viongozi wa dini pamoja na waserikali kuwekeza katika sekta ya madini ili waweze kufaidika na madini yaliyopo Tanzania,  waweze kukua kiuchumi na kukuza uchumi wa Tanzania kwa ujumla na kuweza kuongeza kiwango cha mabilionea.

“Napenda nichukue fursa hii kuendelea kuwakaribisha wawekezaji ndani na nje ya nchi kuwekeza hapa nchini, serikali ninayoiongoza haiwachukii wawekezaji ila ina wapenda wawekezaji na ndio maana tuliingia kwenye makubaliano na kampuni ya kimataifa ya Barrick. Anaetaka kuwekeza anakaribishwa sana.” amesema Magufuli.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Madini Mheshimiwa  Doto Biteko amempongeza na kumshukuru Mhe.Rais Magufuli kwa jitihada alizofanya na kuweza kuibadilisha sekta ya madini  na kufanya wachimbaji wa madini wawe na uhakika wa soko, zaidi kwa kuifanya Tanzania kuwa kituo kikuu cha kuuza madini

“Mheshimiwa Rais sekta hii ya madini imebadilika sana na kama kuna mtu mmoja aliyeibadilisha sekta hii ni wewe, mambo yote yanayotokea kwenye sekta hii yasingeweza kutokea kama kusingekuwa na utashi na msukumo mkubwa ambao umekuwa ukifanya toka ulivyoingia madarakani na kwa michakato mbalimbali ambayo wewe mwenyewe umeisimamia na ambayo umekuwa ukitupa mar azote pale wizarani tunakushukuru sana Mhe.Rais na Mungu akubariki sana” amesema Mhe.Biteko.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments