Majaliwa: Mchagueni Dkt. Magufuli, Anaweza Kudumisha Muungano


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Zanzibar wamchague Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa kudumisha Muungano.

“Nawaletea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya makubwa kwenye uongozi wake uliopita. Hata kwenye wizara alizowahi kuongoza, pia amefanya makubwa. Ndiye mgombea pekee mweye uwezo wa kutuunganisha Wazanzibari na Watanzania Bara,” amesema.

Ametoa wito huo jana (Jumatatu, Oktoba 12, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Kairo, Kiwengwa, wilaya ya Kaskazini B.

Amesema wako baadhi ya wagombea ambao wanatangaza kuuvunja muungano pindi wakichaguliwa na amewataka wakazi hao wawaepuke. Amesisitiza kuwa kazi ya Urais si ya mchezo na inataka mtu makini, kwa hiyo akawaomba wakazi hao wamchangue mtu ambaye ana uwezo wa kupambana na wala rushwa.

Mheshimiwa Majaliwa yuko Zanzibar kuwaombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ally Mwinyi, wagombea ubunge wa majimbo mbalimbali, wawakilishi na wagombea udiwani.

Akimuombea kura Dkt. Mwinyi, Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama cha Mapinduzi kina benki ya kutosha ya makada wenye uwezo wa kuongoza. “Chama cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za uongozi, na katika nafasi hii ya kuongoza Zanzibar, tumemleta Dkt. Hussein Mwinyi.”

Amesema yako mambo mengi mazuri yamefanywa na Dkt. Ali Mohammed Shein na yaliyobakia yatakamilishwa na Dkt. Hussein Mwinyi. “Masuala yote ya kipaumbele yamewekwa kwenye ilani ya uchaguzi ya yenye kurasa 303. Pia kitabu hiki kimesambazwa hadi kwenye shehia zenu. Kitafuteni mkisome ili muone mambo yaliyopangwa kufanyika kwa ajili ya Zanzibar.”

“Maendeleo ya mifugo yamo humu, maendeleo ya uvuvi yamo humu, maendeleo ya ajira yamo, kuwezesha sekta binafsi yamo humu, kuwezesha viwanda yamo humu, kuwezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa nayo pia yamo humu,” ameeleza.

Mapema, akinadi sera zake, Dkt. Hussein Mwinyi alisema Serikali yake itaimarisha uvuvi wa bahari kuu pamoja na bandari za uvuvi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki ili kuongeza ajira na masoko kwa bidhaa za baharini.

Alisema ataimarisha ufugaji wa samaki ikiwa ni njia mojawapo kuu ya kulinda mazingira. “Nitasimamia hilo la ufungaji wa samaki hasa kwenye maeneo ya mikoko kwa sababu tutakuwa pia tunalinda mazingira yetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa atashughulikia tatizo la mmomonyoko wa maadili na hasa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji wa wanawake na watoto. “Ninaowaomba mtoe ushirikiano kwa sababu wanaofanya hivi vitendo mnawajua. Tusaidieni ili tuweze kudhibiti hivi vitendo vya udhalilishaji na dawa za kulevya,” alisema.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, Dkt, Mwinyi alisema upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 72 na kwamba asilimia 28 iliyobakia ni ya kutoa maji kutoka barabara kuu hadi kwenye makazi ya watu. “Serikali yetu itakamilisha hiyo sehemu ndogo iliyobakia,” alisema.

Dkt. Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kuomba kura za Dkt. Magufuli, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa CCM.

 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments