BENKI YA CRDB YAWEKEZA SH. BILIONI 7 NDANI YA KCBL | MALUNDE 1 BLOG

Thursday, October 22, 2020

BENKI YA CRDB YAWEKEZA SH. BILIONI 7 NDANI YA KCBL

  Malunde       Thursday, October 22, 2020

 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amiepongeza Benki ya CRDB kwa kuchukua hatua ya kuifufua Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) na hivyo kutoa tumaini jipya kwa vyama vya ushirika nchini ambao ni wadau wakubwa wa benki hiyo. Naibu Waziri Kijaji ametoa pongezi hizo katika hafla ya uzinduzi wa huduma za Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) iliyofanyika katika makao makuu ya benki hiyo mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Benard Kibese. 


Naibu Waziri Kijaji amesema kuwa ushirika ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dokta John Pombe Magufuli imejidhatiti katika kuhakikisha mwelekeo wa jumla wa Ushirika katika siku za usoni unaiongoza jamii ya Watanzania kufikia malengo ya maendeleo endelevu.


“Kama Naibu Waziri mwenye dhamana ya sekta ya fedha nchini nimefurahishwa sana na uamuzi huu wa Benki ya CRDB kuweka mtaji katika Benki hii ya KCBL ambayo kwetu sisi tunaitazama kama Benki Kuu ya Ushirika katika siku za usoni na ni imani yangu kuwa uwekezaji huu utakwenda kuifanya Benki ya KCBL kuwa na ushindani zaidi kwenye soko na hivyo kuleta tija sio tu kwa Serikali bali kwa Watanzania kwa ujumla” alisema Naibu Waziri Kijaji.


Naibu Waziri Kijaji amewasihi watendaji wa Benki ya KCBL kuhakikisha kuwa wanakwenda kusimamia vyema rasilimali na benki hiyo na kutokua na mchezo na wote ambao wanaonyesha kutokua na nia njema na benki hiyo ili kutoirudisha benki hiyo ku. Sambamba na hilo Waziri Kijaji ameiomba Benki ya KCBL kuweka mikakati ya kutoa elimu kwa wateja ili kuchochea upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania wengi zaidi hususan ambao wapo kwenye ushirika. 


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB na , Bw. Fredrick Nshekanabo amewaomba wateja, vyama vya ushirika, akiba na mikopo, na wadau wote wa KCBL kurejesha imani kwa benki hiyo kwani sasa Benki ya CRDB inakwenda kuirejesha kwenye ramani kupitia uwekezaji wa mtaji pamoja na rasimali watu. Kaimu Mkurugenzi huyo amesema kuwa wanaamini uzoefu wa Benki ya CRDB katika masuala ya ushirika kutokana na chimbuko lake kuwa kwenye ushirika utakua chachu kubwa katika kuifufua benki hiyo kama ambavyo wameweza kufanya kwa Benki ya TACOBA ambayo ilipitia kipindi kigumu kama ilivyo kwa Benki ya Ushirika Kilimanjaro na sasa inafanya vizuri na kupata faida. 


“Siku zote ahadi yetu kwa serikali ni kuwa “TUPO TAYARI” kushiriki katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu ya Tanzania. Na leo naomba kurudia tena kuwa “TUPO TAYARI” kuhakikisha tunairudisha KCBL kwenye ramani na kuipa sura mpya ambayo itakua na tija kwa wadau wake wote. Nakuomba utufikishie salamu kwa Mh. Rais kuwa jambo hili la KCBL tumelichukua na kwa lugha ya sasa tunasema hili ni “JAMBO LETU” na tutakwenda nalo ije mvua lije jua hadi kulifanikisha” alisema Nshekanabo. 

 

Katika uwekezaji huo Benki ya CRDB imewekeza mtaji wa Shilingi Bilioni 7 ili kuongeza mtaji na ukwasi kwa Benki ya KCBL ambayo ilipitia kipindi kigumu kifedha kutokana na ubadhilifu wa baadhi ya watendaji wake na kupelekea benki hiyo kusimamisha shughuli za uendeshaji. Sambamba na mtaji huo Benki ya CRDB itatoa rasilimali watu ili kusimamia uendeshaji wa Benki ya Ushirika Kilimanjaro ambapo Benki ya CRDB itatoa watendaji wanne katika nafasi za nafasi za Meneja Mkuu, Mkuu wa Idara ya Fedha na Uendeshaji, Mkuu wa Idara ya Mikopo na Ukuzaji wa Biashara pamoja Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani pamoja na wajumbe wawili wa Bodi.  


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira amesema Benki ya Ushirika ya KCBL haikufa yenyewe kutokana na sababu za kibiashara bali iliuawa na watu ambao hawakua na dhamira njema kwa benki hiyo pamoja na ushirika nchini. Amesema mchakato wa kuifufua Benki ya KCBL haukua rahisi lakini kutokana na juhudi za Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania mchakato huo umewezekana huku pia akishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha wote walioshiriki katika kuiua benki hiyo wanafikishwa mbele ya sheria.


Nae Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Benard Kibesse ameipongeza Benki ya CRDB kwa uwekezaji huo na kusema kuwa benki nyingi nchini hazikua tayari kuwekeza katika benki hiyo lakini Benki ya CRDB iliweza kuchukua uamuzi huo kutokana na yenyewe kuwa ni zao la ushirika kama ilivyo Benki ya KCBL. Dkt. Kibese amesema pamoja na uwekezaji huo kwa Benki ya CRDB lakini haifanyi kuwa Benki ya KCBL kuwa mali ya Benki ya CRDB bali benki hiyo itabaki kuwa ya ushirika kama dhamira ya kuianzisha ilivyokua.  
Kuhusu Benki ya CRDB

Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo.


Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. 


Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania na Burundi kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni 3 na kupitia mtandao mpana wa matawi 268, zaidi ya CRDB Wakala 15,000, 537 ATM, mashine za manunuzi 1,200 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Jina

Namba ya Simu

Barua Pepe

TullyEsther Mwambapa

+255 769 200 600

Tullyesther.Mwambapa@crdbbank.comUsikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post