MVUA YAUA WATU 12 DAR... HAYA HAPA MAJINA YAO

 

Na Heri Shaban, TimesMajira,Online Dar es salaam

WATU 12 wamefariki katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na mvua iliyoanza kunyesha saa 10 alfajiri ya Oktoba 13, mwaka huu na kuendelea kunyesha vilivyotokana na athari ya mvua inayoendelea kunyesha mchana kutwa nzima.

Mbali na vifo hivyo vilivyosababishwa na mvua, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imetaja majina ya watu watano wa familia moja waliokufa baada ya nyumba yao kuungua moto katika tukio lililotokea Pungu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kutokea kwa vifo hivyo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo.

Amesema vifo hilivyosababishwa na athari za mvua vilitokea katika Mikoa ya Kipolisi Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam.

Amewataja waliofariki Mkoa wa Kipolisi Ilala kuwa ni Mariam Yahaya (45) Herieth Kanuti (18) mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Lutihinda na Ipyana Mwakifuna(19) Mkazi wa Jangwani, Askari Jeshi la akiba la Mgambo.

Amesema miili mingine ya watu watatu bado haijatambuliwa, ambapo wanaume ni wawili na mwanamke mmoja. Aidha, amesema tukio lingine la kifo limeripotiwa juzi majira ya saa 12.45 asubuhi maeneo ya Tabata, ambapo mwili wa mtu mmoja mwanaume aliyefahamika kwa majina ya Philipo Feliciani (30), mkazi wa Tabata Kimanga, ulionekana ukiwa umenasa kwenye matope katika mto Tenge, ambaye alifariki dunia Oktoba 13,2020 saa 12 jioni.

Pia amesema mwili wa mtu mmoja mwingine mwanaume asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30-35 alikutwa akiwa amefariki dunia katika eneo la Ukonga Sabasaba Mji Mpya.

Kwa upande wa Kinondoni, amesema watu wanne wamefariki kutokana na mvua hizo.

Kwa mujibu wa Mambosasa kati ya waliofariki, watoto wawili ni wa familia moja na watu wazima wawili.

Amewataja waliofariki Ibrahim Hassani (24) mkazi wa Kigogo Buyuni, Hussein Awadhi (5) mkazi wa Kigogo Buyuni na Bakari Awadhi (14), mkazi wa Kigogo Buyuni.

Amesema watoto hao walifariki dunia kwa kusombwa na maji baada ya nyumba yao iliyopo katika Bonde la Kigogo kujaa maji na watoto hao kushindwa kujiokoa.

Ameongeza kuwa marehemu Ibrahim Hassani alijaribu kumuokoa mtoto mmoja, lakini na yeye alisombwa na maji na kufariki dunia.

 CHANZO- MAJIRATIMES

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments