RPC SHINYANGA AZUNGUMZIA TUKIO LA OFISI ZA CHADEMA KUDAIWA KUNUSURIKA KUCHOMWA MOTO ....."TUNAMSHIKILIA MLINZI"


Muonekano wa vioo vya dirisha la Ofisi ya CHADEMA Kanda ya Serengeti, Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la ofisi ya CHADEMA Kanda ya Serengeti iliyopo Majengo Mapya mjini Shinyanga kuvunjwa na watu ambao hawajafahamika usiku wa kuamkia leo Jumapili Oktoba,2020. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema katika eneo la tukio kumekutwa chupa moja yenye ujazo wa lita 1.5 yenye kimiminika kidhaniwacho ni mafuta ya petroli ndani yake ikiwa na utambi. 

“Mnamo tarehe 25/10/2020 majira ya saa kumi alfajiri huko katika ofisi za CHADEMA Kanda ya Serengeti zilizopo Majengo mapya, kata ya Ngokolo, Manispaa na mkoa wa Shinyanga Joseph Ndatala (43), Afisa Organization Mipango na Uchaguzi CHADEMA, mkazi wa Ndala aligundua kioo cha dirisha la ofisi ya ofisa wa organization na uchaguzi kuvunjwa na mtu/watu ambao bado hawajafahamika”,amesema Kamanda Magiligimba. 

Amesema mtuhumiwa mmoja anashikiliwa kwa mahojiano zaidi ambaye ni Edward Andrea (46), na mlinzi wa Shiroh Security Ltd ambaye ni mlinzi wa ofisi hizo za CHADEMA Kanda ya Serengeti. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo asubuhi Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amesema: 

“Leo majira ya saa saba usiku ofisi yetu ya Kanda ya Serengeti imenusurika shambulio la kuchomwa moto. Tulipewa taarifa na walinzi wetu kwamba kioo cha dirisha la ofisi ya Katibu kimevunjwa.

Na baadaye tumejaribu kuangalia labda ni vibaka walitaka kuiba lakini tulivyoingia ndani tukakutana na hali ambayo inaonesha kulikuwa na watu wenye nia ovu ya kulipua kwa petroli. Tumekuta chupa yenye mafuta ya petroli kiasi cha lita moja na nusu na utambi ndani na ukiwa umeunguzwa kidogo ikionesha kwamba huyo mtu alikuwa amewasha moto na bahati nzuri moto huo haukuwaka”,ameeleza Mnyawami. 

“Tunalishukuru sana jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano wa kutosha waliotupatia. Mtu wa kwanza kufika hapa baada ya sisi kutoa taarifa polisi ni OCD pamoja na askari wake. Lakini pia nimshukuru Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Shinyanga amefika eneo la tukio kujionea hali halisi. Polisi wametoa ushirikiano mzuri na mambo mengine ya Kiupelelezi tumewaachia wao”,amesema Mnyawami.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments