YAJUE MAJUKUMU YA NEC KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA, 2020


 Na.Beatrice Sanga-MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) ipo kisheria kwa mujibu wa Katiba chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na lengo lake ni  kuratibu na kusimamia uendeshaji Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Madiwani kwa Tanzania Bara. Kupitia uandikishaji  wa wapiga Kura, ugawaji wa majimbo na utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha demokrasia, NEC inatekeleza wajibu huo ili kuwawezesha wananchi kufanya zoezi la kuchagua viongozi wao.


Katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku NEC ina mfumo wa uchaguzi unaotumika katika kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani, ambapo mgombea anayepata kura nyingi na halali kuliko wenzake ndiye hutangazwa kuwa mshindi. NEC pia hutoa miongozo na taratibu mbalimbali za uchaguzi ili kuweza kufanikisha suala zima la uchaguzi.

Tunapoelekea katika Uchaguzi  Mkuu  utakaofanyika tarehe 28,Oktoba,2020 ni muhimu sana Watanzania na wapiga kura wote wakapata elimu itakayo waongoza katika kufanikisha mchakato mzima wa kupiga Kura, kuwaelimisha wananchi kuhusu mambo ya msingi  yatakayowawezesha  kutekeleza  jukumu hilo la kikatiba ambalo litafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Wananchi wanapaswa kujua na kupewa elimu ya nani anaruhusiwa kupiga kura, wapi anaweza kupiga kura, kituo cha kupigia kura, muda wa kupiga kura, mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kupiga kura na jinsi ya kupiga kura. Hii itawawezesha  wananchi kuwa na uelewa mpana utakao wasaidia wakati  wa kutekeleza zoezi  la upigaji kura.

Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania inampa haki kila raia aliyetimiza miaka 18 kupiga  kura. Kwa  mujibu wa vifungu vya 13(1), 13(2), 35C, 61 (3)(a) na 63(1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani), Sura  ya 292, ili mtu aweze kupiga kura na kumchagua kiongozi anayemtaka ni lazima awe amejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwa  na kadi ya mpiga kura iliyotolewa na NEC.

Aidha, mwananchi anatakiwa kuwepo katika kituo alichojiandikishia kwa sababu ndipo jina na taarifa zake zitakapoonekana. Katika maeneo na vituo mbalimbali vya kupigia kura, Tume itabandika orodha ya majina ya wapiga kura ili kila mwananchi aweze kujua ni kituo gani atapigia kura, hata hivyo kwa sintofahamu yoyote ambayo mtu anaweza kuipata kutakuwa na makarani waongozaji katika kila kituo cha kupigia kura ili kuwasaidia wapiga kura kutambua vituo vyao na mambo muhimu kuhusu mchakato mzima wa kupiga kura.

Hata hivyo  mpiga kura anatakiwa kufika kituoni katika muda uliotangazwa ambapo  kwa mujibu wa NEC, siku ya uchaguzi vituo vyote vya kupigia kura vitakuwa wazi  saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni kwa Tanzania Bara.  Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, vituo vitakuwa wazi kuanzia saa moja kamili  asubuhi na kufungwa saa kumi na moja kamili jioni. Muda huo ukiisha hakuna mtu  atakayeruhusiwa kuingia kwenye mstari kwa ajili ya kupiga kura.

Kila raia anapaswa kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi ili kuweza kuepuka sitofahamu yoyote inayoweza kujitokeza  katika kituo cha kupigia kura na kufanya mtu kukosa haki yake ya msingi ya kumpigia kura kiongozi anayemtaka.  Aidha NEC inapaswa kuendelea kutoa Elimu, kuratibu na kusimamia watu wanaotoa elimu hiyo ya uchaguzi kama ilivyoainishwa  katika Kifungu cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi , Sura ya 343, na Sheria ya Uchaguzi  wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Tanzania inafanya uchaguzi wa sita tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza kutumika. Vyama vilivyochukua fomu kwa ajili ya kugombea kiti cha Urais in 17 ambapo vyama vilivyoteuliwa na NEC kugombea nafasi hiyo ni 15. Wagombea wa vyama viwili walienguliwa na Tume kutokana na kutokidhi vigezo. Jumla ya wapiga kura 29,188,347 wamejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo 80,155 vitatumika katika shughuli ya kupiga kura.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post