WIZARA YA ARDHI YAZINDUA SIKU MAALUM YA MLIPA KODI


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua rasmi siku Maalum ya Mlipa Kodi ya Pango la Ardhi itakayoendeshwa katika mikoa yote ya Tanzania.



Uzinduzi huo ambao ni mkakati maalum wa Wizara ya Ardhi kuhamasisha wamiliki wa ardhi kulipa kodi ya pango la ardhi ambapo na utekelezaji wake ulianza mwishoni mwa wiki mkoani Dodoma kwa Maofisa Ardhi wa Makao Makuu kwa kushirikiana na wale wa ofisi za ardhi za mikoa na  wa jiji la Dodoma kutembelea mitaa ya Kisasa na Ilazo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami, zoezi hilo la siku ya Mlipa Kodi ya Pango la Ardhi litakuwa likifanyika kila siku ya Ijumaa kwa Maafisa wote wa Ardhi nchi nzima kutembelea mitaa mbalimbali nyumba kwa nyumba kwa lengo la kutoa elimu na kutatua changamoto za ardhi.

‘’Zoezi hili litakuwa likifanyika kila siku ya Ijumaa na litahusisha maafisa wote wa ardhi katika mikoa ya Tanzania Bara na hapa Maafisa Ardhi hawatakiwi kujionesha wao ni nani kinachotakiwa ni kutoa elimu na leo tumeanza jiji la Dodoma kama uzinduzi rasmi wa siku hiyo’’ alisema Denis Masami.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi alisema, mbali na zoezi hilo la kutembelea wamiliki wa ardhi nyumba kwa nyumba kutatua changamoto za ardhi pia llitatumika kuhuisha kumbukumbu za  ardhi kwa wamiliki na kukagua uendelezaji miji.

Masami amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanaacha mawasiliano sahihi majumbani mwao ili maofisa ardhi watakapopita na kuwakosa waweze kuwasiliana kwa njia ya simu ili kupata taarifa sahihi zitakazowezesha uhuishaji kumbukumbu za ardhi kwa wamiliki.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleoi ya Makazi kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200 ya kodi ya Pango la Ardhi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527