Orodha Kamili Ya Viti Maalum Ubunge Na Udiwani Kutolewa Baada Ya Ushiriki Wa Kampeni


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ametoa msimamo wa Chama katika kuteua wabunge wa viti maalum, ambapo ameeleza kuwa, kwa upande wa Udiwani aliyeshinda kura za maoni ndio atateuliwa, isipokuwa kama itadhihirika ushiriki wake wa kampeni haukuwa wa kuridhisha.

Ameyasema hayo  tarehe 18 Septemba, 2020 katika kikao cha viongozi wa CCM wa ngazi ya mashina, Matawi, Kata na Wilaya ya Bukoba Mjini.

*"Kwa wagombea wa viti Maalum, Udiwani na Ubunge, orodha kamili itatolewa baada ya tathmini ya ushiriki wao katika kutafuta kura",*

Amesisitiza kuwa, *"wakati wa kura za maoni za udiwani wa viti maalum, halmashauri kuu za mikoa ndio zilikuwa zinafanya uteuzi wa mwisho wapo baadhi ya viongozi wamechezea matokeo ya kura za maoni na kuwaonea walioshinda kura za maoni kwa visingizio visivyokuwa na kichwa wala miguu,"*

Katibu Mkuu, ametumia wasaa huo katika kikao hiko cha ndani, kutoa msimamo wa Chama kuhusu madiwani hao wa viti maalum,

*"Aliyeshinda kura za maoni za udiwani ndiye anayeteuliwa, aliyeongoza kura za maoni Udiwani viti maalum, ndiye anayeteuliwa mpaka itakapothibitika kuwa ushiriki wake katika kuomba kura haukuridhisha.., kuna mkoa mmoja  hawakuchukua wakwanza mpaka watano, eti kwa sababu hawakuchangia asilimia 10, zile pesa ni za hiyari sio lazima."*

*"Kanuni zetu zinasema, kura za maoni, sio kigezo pekee cha uteuzi lakini kuongoza kura ni kigezo muhimu sana mpaka upate sababu zenye ushahidi na zenye kusimamia uhai wa chama ndipo usimteue."* Dkt. Bashiru amefafanua.

Aidha, Katibu Mkuu pamoja na mambo mengine, amekemea vikali, tabia za baadhi ya wanaCCM wanaopanga kikisaliti chama katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa maslahi yao binafsi,

*"Sasa nawahakikishia msaliti na mnafiki akibainika hatutamgusa wakati wa vita na msiwaguse hawa wakati wa vita, Wakati wa vita sio wakati wa kugombana, lakini tusizushiane tukawachonga wasaliti tukawachonga wanafiki kumbe watu wanaonewa."*

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa, *"Tutajiridhisha kwa ushahidi na tunaendelea kushughulika nao, tukimaliza uchaguzi, wanafiki watasafishwa wote kwenye chama chetu, hata kama una urefu kama mnara wa baberi tutakuangusha."*

Awali kabla ya kikao hiko, Katibu Mkuu kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM na Mgombea Urais na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, amehudhuria hafla ya kuaga miili ya marehemu Kumi wanafunzi wa shule ya Msingi Byamungu vilivyotokea Septemba 14, 2020 kwa ajali ya moto Wilayani Kyerwa.

Vikao hivyo, ni mfululizo wa ujenzi na uimarishaji wa mshikamano, nidhamu, na moyo wa kujitolewa hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu, ili kijihakikishia ushindi Mkubwa kwa CCM.

Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post