DKT. ZAINABU CHAULA ATUNUKU VYETI KWA WAHITIMU WA MAFUNZO YA TEKNOLOJIA YA 5G

Na Faraja Mpina, WUUM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainabu Chaula ametunuku vyeti kwa wahitimu 24 waliopatiwa mafunzo ya teknolojia mpya ya 5G yaliyotolewa na Kampuni ya simu ya Huawei Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano uliopo Mji wa Serikali, Mtumba mkoani Dodoma.

Wahitimu wa mafunzo hayo ni wataalamu watano 5 kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), wataalamu 8 kutoka  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wataalamu 10 kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na mtaalamu mmoja kutoka Tume ya Taifa ya TEHAMA.

Dkt. Zainabu Chaula amewapongeza wahitimu kwa kumaliza mafunzo hayo ambayo yamefanyika nje ya muda wa kazi na kuwashukuru Huawei Tanzania kwa ushirikiano wao endelevu na  kuwawezesha watumishi wa Sekta ya Mawasiliano pamoja na taasisi zake kuifahamu teknolojia mpya ya 5G.

Dkt. Chaula amesema kuwa kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA yenye kasi zaidi, itawezesha Serikali kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza makusanyo ya mapato ambayo yataliwezesha Taifa la Tanzania kutoka uchumi wa kati na kwenda katika uchumi wa juu.

Naye Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Mhandisi Aweso Aweso ambaye ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo amesema kuwa, teknolojia mpya inapotambulishwa ni jukumu la wataalamu wa Serikali kujifunza na kuielewa ili kuwawezesha katika kutunga Sera, ambazo zitasaidia kusimamia mwenendo mzima wa miundombinu ya TEHAMA na matumizi ya huduma za mawasiliano.

Aliongeza kuwa teknolojia ya 5G ni teknolojia yenye sifa za ziada kwa sababu ina akisi akili za binadamu, hivyo itasaidia Serikali kutoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi wake kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye kasi.

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huawei Tanzania, Damon Zhang amesema Tanzania imeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya TEHAMA kwa kuhakikisha kila kona ya nchi imefikiwa na miundombinu hiyo, hivyo nchi kuweza kuleta mabadiliko ya kweli na  kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya TEHAMA amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano ina jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye viwango bora zaidi, na mafunzo yaliyotolewa na kampuni ya Huawei Tanzania ni hatua nzuri ya kuwajengea uwezo wataalamu ili kuleta ushindani na mataifa mengine.

Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Mulembwa Munaku amesema kuwa mafunzo hayo ya teknolojia ya 5G ambayo yametolewa na Kampuni ya Huawei Tanzania kwa wataalamu wazalendo watanzania ambapo yamejikita katika masuala yanayohusu teknolojia mpya ya 5G katika usimikaji wa miundombinu,  usambazaji wa huduma za mtandao, mahitaji ya mpangilio na mgawanyo wa masafa,  mpango wa biashara na usimamizi wa teknolojia mpya ya 5G.

Munaku ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya teknolojia mpya ya 5G kwa wataalamu wengine wa Serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na teknolojia mpya.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527