WAITARA AZINDUA KAMPENI TARIME VIJIJINI ....ATAJA AHADI 13 ATAKAZOTEKELEZA AKISHINDA UBUNGE


Wanachi wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea Ubunge jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara

Na Dinna Maningo,Tarime.
Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mwita Waitara, amezindua kampeni huku akiahidi kuleta maendeleo na kutatua kero za wananchi.

Waitara aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za kugombea ubunge wa jimbo hilo ambapo viongozi mbalimbali wa CCM, akiwemo Mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki, Wagombea nafasi za Udiwani na Wananchi walishiriki katika uzinduzi.

Waitara akiwa ameongozana na wana CCM na wananchi waliichapa mwendo wa km 5 kwa kutembea kwa miguu kutoka Kijiji cha Muriba hadi viwanja vya mkutano wa Uzinduzi kijiji cha Nyamwaga ambapo shangwe,furaha burudani mbalimbali ikiwemo ngoma ya asili ya Litungu vilitawala.

Waitara alitaja baadhi ya mambo atakayoshughulikia iwapo wananchi watamchangua kuwa mbunge wa jimbo hilo, ambapo alisema kuwa katika ubunge wake atahakikisha barabara inayopita katika jimbo hilo ikitokea Tarime kwenda Serengeti inajengwa kwa kiwango cha lami.

Ahadi ya pili aliyoitoa Waitara ni  kutatua mgogoro kati ya koo ya Wanyamongo na Wairege.

Ahadi ya tatu alisema kuwa licha ya wafanyabiashara kwenye masoko na stendi kuchangia mapato halmashauri lakini maeneo mengi hayana huduma ya choo.

" Ukienda Nyamongo hakuna choo cha stendi wala cha soko,Sirari hivyo hivyo ili upate huduma mpaka ukimbie nyumbani au kwenye miji ya watu kuomba huduma mkinichagua nitahakikisha kwenye masoko na stend choo zinajengwa",alisema.

Ahadi ya nne alisema atahakikisha anachimba visima kwenye maeneo ya umma zikiwemo shule za msingi na Sekondari,vituo vya afya ili kuondokana na adha ya ukosefu wa huduma ya maji.

Ahadi ya Tano,Waitara alisema kuwa baadhi ya vijiji havina umeme kikiwemo Kijiji cha Kiterere ambacho kuna Zahanati lakini hakuna umeme na hivyo kusababisha watoa huduma ya afya na wagonjwa kutumia vibatari.

Ahadi ya sita alisema kuwa kumekuwa na mahusiano mabaya katika mpaka wa Sirari juu ya wafanyabiashara wanaovusha bidhaa kupitia mpaka huo,Wanyamongo na Mgodi wa dhahabu wa Barrick na Wananchi wanaopakana na Hifadhi ya wanyama ya Serengeti.

"Nitajenga mahusiano mazuri ili kuondoa migogoro katika mpaka wa Sirari,Nyamongo na wananchi wanaopakana na TANAPA", alisema

Waitara alisema kuwa ahadi ya Saba atahakikisha mji wa Nyamongo unapata maji safi na salama na barabara zake kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na ajira.

"Nyamongo haipaswi kuwa na maisha magumu na wakati wana Mgodi unaoiingizia Serikali mabilioni ya fedha,barabara za Nyamongo zilipaswa kuwa za lami, tatizo la ukosefu wa ajira wananchi wamekuwa wakiulalamikia mgodi kutowapa ajira hivyo nitahakikisha ajira zinapatiakana ili kuondoa malalamiko", alisema Waitara.

Waitara alisema kuwa ahadi ya nane nikuhakikisha utekelezaji unafanyika wa Sirari kuwa mamlaka ya mji mdogo kama ilivyoagizwa na Mizengo Pinda aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye aliyeagiza Sirari kuwa mamlaka ya mji mdogo lakini mpaka sasa agizo hilo halikutekelezwa.

Waitara alisema ahadi ya 9 atahakikisha zao la Kahawa linapata soko la uhakika, ahadi ya 10 ni kuwezesha kata ya Kiore,Bumera na Susuni zinarudishwa katika halmashauri ya mji Tarime kutokana na kwamba wananchi wa maeneo hayo wanatumia gharama kubwa kwenda kupata huduma halmashauri ya wilaya iliyopo kata ya Nyamwaga.

Alisema ahadi ya 11 ni kuipandisha hadhi shule ya Sekondari Inchugu kuwa na elimu ya kidato cha tano na sita,ahadi ya 12 ni kuhakikisha kinajengwa Kituo cha Afya kata ya Nyarero,na ahadi ya 13 alisema akiwa mbunge atahakikisha inatungwa sheria ndogo juu ya maslahi ya wenyeviti wa vijiji lakini pia kuhakikisha milioni 20 zinakwenda kwenye vijiji ambazo alieleza kuwa fedha zimekuwa zikikusanywa lakini haziendi kwenye vijijini.

Mgombea huyo wa Ubunge hakuishia tu kutoa ahadi lakini pia alieleza mambo aliyofanikisha katika maendeleo ya jimbo la Tarime vijijini akiwa kama Naibu Waziri wa TAMISEMI ikiwa ni pamoja na kuzuia Bilioni 5.7 fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Tarime kutoka Mgodi wa dhahabu wa Nyamongo zilizotakiwa na mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima kuzigawa kwenye wilaya zote za mkoa wa Mara.

"Mimi kama Naibu TAMISEMI nilipambana kuhakikisha nazuia bilioni 5.7 zilizokuwa zigawanywe kwenda halmashauri zingine na wakati ni fedha za mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Aliongeza" Serikali imetoa fedha za maendeleo ikiwemo miradi ya ujenzi kama sh milioni 50 kujenga Bweni Inchugu Sekondari,kituo cha Afya Sirari milioni 500,hiyo ni baadhi ya miradi lakini pia nimechangia fedha zangu za mfukoni kwenye miradi ya ujenzi wa shule ,watu wa Tarime Rais Magufuli anawapenda na ndiyo maana Naibu Waziri na Katibu mkuu wa TAMISEMI wanatoka Tarime naomba mnichague nitafanya mkubwa",alisema Waitara.

Waitara alisema kuwa hizo ni baadhi ya ahadi nakwamba ahadi zingine atazitoa wakati akiendelea na kampeni zake kwenye vijijini mbalimbali huku akiwaomba wananchi kuwapuuza wanaomchafua na badala yake wampige kura na kisha wampime kwa vitendo.

Katika uzinduzi huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime na Diwani wa kata ya Nyamwaga Mosses Misiwa kupitia CHADEMA ambaye alijiunga na CCM alisema kuwa maendeleo ya Tarime vijijini yametekelezwa na halmashauri na Madiwani wa vyama vyoye ambao waliibua vipaumbele nakwamba hayajafanywa na aliyekuwa Mbunge John Heche wa Chadema.

Misiwa alisema kuwa fedha za Ushuru wa Huduma (Service Levy) siyo hisani wala msaada wa halmashauri bali ipo kisheria kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 1982 inayozitaka kampuni zinazofanya kazi ndani ya halmashauri kulipa 0.3 ya mapato yake yote ya mwaka au miezi sita kulingana na ambavyo mmekubaliana. 

" Mgodi ulikuwa ukileta fedha kidogo baada ya timbwili la wananchi bila kuangalia itikadi ya vyama vya siasa nilipoitikisa ile ligi mgodi uliongeza fedha kutoka bilioni 1.5 hadi Bilioni 5 hizo fedha ndiyo zimetengeneza Vituo vya afya,Zahanati na shughuli zingine kwa kushirikiana na Madiwani wenzangu.

Aliongeza"Mbunge ni Diwani kwenye halmashauri baba yao ni Mwenyekiti wa halmashauri kwa hiyo asijitokeze mtu anawadanganya kuwa yeye ndiyo kajenga hivyo vituo vya afya na Zahanati wala kujenga barabara ni uongo",alisema Misiwa.

Alisema kuwa 2015 kabla Chadema haijaongoza jimbo na halmashauri, halmashauri ilikuwa inapata fedha kila mwaka za mfuko wa barabara zaidi ya Bilioni 1.5 kutoka Serikalini lakini Chadema ilipoingia madarakani fedha hizo hazijawahi kutolewa.

"Nategemea wewe Waitara ukiingia pale mambo mengi yatafanyika maana nimeona na nimekufuatilia kwa muda mrefu una mahusiano mazuri na Rais wetu John Magufuli,tangu wale wavurugaji waingie madarakani tumekosa fedha nyingi za ruzuku kutoka Serikali kuu zaidi ya milioni 800", alisema Misiwa.

Misiwa alisema kuwa wakati wa kampeni za Ras Magufuli aliahidi ujenzi wa barabara ya kilomita 87 kwa kiwango cha lami kutoka Tarime mjini hadi Serengeti na ikafanyiwa upembuzi lakini hata hivyo haijajengwa kutokana na kufanya maamuzi mabaya katika uchaguzi wa 2015.

"Ukikosea kuchagua umekosea kupata maendeleo Ibara ya 8 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema Serikali itapata mamlaka yake kutoka kwa wananchi na Serikali hiyo itapanga mahitaji ya wananchi kulingana na wanavyotaka sasa sisi tunaweka Serikali ya JPM tunachanganya na figa fupi jikoni.

"Wakati naingia hapa uwanjani vijana wameniuliza je tumwamini Waitara kama tunavyokwamini wewe? nikawaambia CCM ya leo siyo CCM ya zamani CCM inayoongozwa na na Rais Magufuli ni ya viwango,isiyotaka rushwa,inayochukia rushwa,CCM ambayo imeboresha usafiri wa anga na inaendelea kuboresha usafiri wa Reli na Majini nawaombeni kura zote pigia Magufuli,Waitara na Madiwani wa CCM", alisema Misiwa.

Waliotia nia kugombea ubunge lakini kura hazikutosha wakiwemo wa jimbo la Tarime vijijini na mjini ,Nicodemas Keraryo,Maitarya Maitarya, Dk.Paul Mwikwabe, James Bwire na wagombea wa viti maalumu walimwombea kura Waitara huku aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Serengeti kupitia CHADEMA na kisha kuhama na kujiunga CCM Ryoba Marwa akiwashukia wana CCM kwa madai kuwa baadhi yao ni wanafiki wamekuwa wakiisaliti CCM na kuipigia kura upinzani.

"Niwape siri,wana CCM wengi ni wanafiki mkishamaliza kura za maoni mnagawanyika nimefurahia sana kuwaona akina Gimunta naomba muunganishe nguvu ,mkiona sisi tuliokuwa upinzani tumerudi CCM siyo jambo dogo nilimwambia hata Heche twende kule yeye akasema anakomaa, unakomaa ambapo hakuna!.

"Huyu kiongozi wa chadema lini aliwaletea maendeleo Tarime ?Mwita Waitara ni chuma hata Heche anajua ,ndugu zangu Heche tangu awe mbunge hajawahi kujenga nyumba Tarime anaishi gest,leo nimekuja kwa jambo moja nimekuja kuwaangaia, mimi nilikuwa mgombea ubunge pamoja nakwamba sikuteuliwa namuunga mgombea wangu",alisema Ryoba.

Mgombea Ubunge viti mgombea maalumu Ghat Chomete alisema" mimi najua Tarime mkisema ndiyo ni ndiyo hamna konakona naomba mpeni kura Waitara atatekeleza yote kwakuwa yako kwenye Ilani ya CCM.

Baadhi ya Watia nia katika Ubunge akiwemo Philipo Nyirabu mtia nia jimbo laTarime mjini,Harun Kihengu walisema kuwa kilichopo sasa ni kazi ya kupiga kampeni na anaimani kubwa Waitara atashinda.

Nyerere Mwera alisema"Chama kimetuletea mgombea na mgombea huyo ni Waitara,Mungu akupe nguvu ili ushinde sina wasiwasi na wewe maana changamoto zote za Tarime vijijini unazijua nenda ukatusimamie",alisema.

Peter Busene alisema" mimi ni mjumbe wa kamati ya maadili jimbo la Tarime vijijini kazi yangu ni kulinda maadili mimi nilikuwa upinzani na Waitara pia lakini sisi siyo wajinga CCM ndiyo inayofanya maendeleo kwakuwa ina Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Modikaya Mseti alisisitiza wananchi kuipigia CCM na kwamba barabara na maji vimekuwa kero na ombi lake ni kumchagua Waitara ili asimamie upatikanaji wa fedha za kufanya maendeleo.

John Gimunta yeye aliwatuhumu baadhi ya wana CCM kumchafua kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook huku akisisitiza kuwa ushindi ni lazima.

"Ukiona vyaelewa ujue vimeundwa tunahitaji ushindi wa kishindo,jimbo hili ni tajiri tunahitaji Waitara akafanye kazi,omonto umwihemi ataghokerwa ( mtu anaependa sifa huwa hashindwi)tunaomba ashinde asaidie Bei za Kahawa,maeneo ya uchumbaji,fidia Nyamongo,na mengine mengi.

"Nasikita kuna baadhi ya wana CCM wameunda akaunti na kuanza kunichonganisha mimi na Waitara watu hao wametumia picha zangu nilizorejesha fomu kuna watu wachache wanaotumia jina langu kunichafua maana walizoea kunichafua hata huko nyuma,wote walioniunga naomba wahamie kwa Waitara ili tumuunge tupate ushindi,Waitara naomba watu wote ambao hawakukuunga naomba uwapokee tushirikiane kulikomboa jimbo" alisema Gimunta.

Wazee wa mila kutoka koo 12 za jamii ya Wakurya nao walishiriki uzinduzi huo ambapo walimpatia Waitara Ngao kuashiria ushindi wa ubunge jimbo la Tarime vijijini.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime Daud Ngocho alisema Misiwa ni chuma kipya ndani ya CCM kokote akitumwa atakwenda nakwamba alichelewa kuingia CCM kwani kupitia yeye yangefanyika makubwa.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Samwel Keboye alisisitiza wana CCM kuungana pamoja ili kuyakomboa majimbo yote ya Tarime hatowavumilia wasaliti ndani ya CCM.

Jimbo la Tarime vijijini lina kata 26,Vijiji 85 na vitongoji 500, linagombewa na wagombea kutoka vyama vitatu,CCM akiwa ni Mwita Waitara,John Heche kutoka CHADEMA na Charles Mwera kutoka ACT Wazalendo.
Aliyevaa shati la kitenge ni Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara akitembea kwa miguu na wananchi wakati wakielekea kwenye uzinduzi wa kampeni kijiji cha Nyamwaga.
Waitara akiwa amebeba ngao na mkuki alivyokabidhiwa na wazee wa mila kutoka koo 12 za jamii ya Wakurya wilayani Tarime kama ishara ya ushindi wa Ubunge.
Wazee wa mila koo 12 Jamii ya kabila la Wakurya wilayani Tarime wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara.
Akina mama wakicheza ngoma ya asili ya Ritungu
Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime Daud Ngocho akiwatambulisha waliokuwa wanachama wa Chadema na kutimkia CCM
Aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime na Diwani wa kata ya Nyamwaga na kisha kupitia chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) Moses Misiwa akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara

Vijana wa Nyamongo wakishangilia uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara
Vijana wa Nyamongo wakishangilia uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara
Wananchi wakionyesha bango
Waliosimama mbele ya jukwaa ni wagombea Udiwani kata mbalimbali jimbo la Tarime vijijini kupitia chama cha Mapinduzi
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea Ubunge Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527