SPIKA NDUGAI AZINDUA KAMPENI JIMBO LA KONDOA


Mitano tena! Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Job Ndugai akiwaomba wananchi wa Kondoa kumpa miaka mitano tena mgombea wa Urais wa CCM, Dk John Magufuli ili aweze kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.
Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu, Job Ndugai akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kondoa Mji waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa jimbo hilo, Makoa Ally ambapo Ndugai ndio alikua mgeni rasmi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Msanii wa Bongo Fleva, Keisha akimuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, mgombea Ubunge wa Kondoa Mji, Makoa Ally na Madiwani wote wa CCM.
Wananchi mbalimbali wa Wilaya ya Kondoa ambao wamejitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Kondoa Mji, Makoa Ally.

Charles James, Michuzi TV

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kondoa kimezindua rasmi kampeni zake za mgombea Ubunge wa Jimbo la Kondoa Mji, Makoa Ally ambapo mgeni rasmi alikua Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Job Ndugai.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Spika Ndugai amewaomba wananchi wa Kondoa wasifanye makosa katika kuchagua wawakilishi wanaojua kero zao na wenye kuweka mbele maslahi yao ili waweze kuwasemea.

Amesema changamoto ya maji waliyonayo wilayani hapo itamalizwa endapo wananchi hao watajitokeza kwa wingi kumpigia kura za kishindo mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, wabunge wa majimbo mawili ya Wilaya hiyo, Makoa Ally wa Kondoa Mji na Dk Ashatu Kijaji wa jimbo la Kondoa.

" Ndugu zangu nyie wote mmejionea jinsi Dk Magufuli alivyoufanya mkoa wetu wa Dodoma kupanda chati, uchumi wetu sasa hivi umekua baada ya kuwa makao makuu ya serikali huku yeye mwenyewe akihamia hapa, nini cha kumpa zaidi ya kura za kishindo?

Mimi ndio Spika wa Bunge, nawajua wabunge wote, hao wapinzani hawajawahi kuwatakia maendeleo watanzania maana wao kila kitu hupinga tu, wanasema Rais anatumia hela hovyo kununua Ndege lakini kesho utawakuta wamezipanda, wanatumia barabara za lami kwenye kampeni zao lakini wanasema hakuna lililofanyika.

Kondoa ni wakati wa kuamka na kutoa kura nyingi za kuwafanya wapinzani wajute kwanini wameshiriki uchaguzi huu, niwahakikishieni mkimleta Makoa bungeni nitamsaidia sana katika kuwaletea maendeleo," Amesema Ndugai.

Kwa upande wake mgombea Ubunge wa Jimbo hilo la Kondoa Mji, Makoa Ally amesema anafahamu changamoto nyingi zinazowakabili wananchi wa Kondoa lakini kero ya Maji ndio kipaumbele chake cha kwanza.

" Najua kuna mambo mengi ya kufanya ila nyinyi wenyewe ni mashahidi kwamba hakuna jambo la muhimu Kondoa kwa sasa kama Maji, niwaombe nipeni ridhaa ya kuwa Mbunge wenu nikashughulike na maji ili dhana ya kumtua mwanamama ndoo kichwani iweze kutumia," Amesema Makoa.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na msanii wa Bongo Fleva, Keisha amewaomba watanzania na wananchi wa Kondoa kuchagua mafiga matatu ya CCM ili yaweze kufanya kazi kwa ushirikiano na kusukuma gurudumu la maendeleo mbele.

" Chagueni Rais, Wabunge na Madiwani wetu, msipowachagua wote kwa pamoja mnakwamisha maendeleo maana wapinzani wale ni kupinga tu sasa watu wanaopinga maendeleo ni ngumu kuikumbusha serikali iwajengee visima vya maji maana wao wanasubiri serikali ijenge ili wapinge, naombeni msifanye kosa Oktoba 28, kura zote kwa CCM," amesema Keisha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post