WANNE WANASWA LIVE KWENYE HARUSI WAKIMUOZESHA MWANAFUNZI WA DARASA LA 5, MIAKA 12 SHINYANGA



Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog 
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashilikilia watu wanne baada ya kuwanasa Mubashara 'Live' kwenye sherehe ya harusi wakimuozesha mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Samuye katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga aliyetolewa mahari ya ng’ombe nane na shilingi 600,000/=. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 14,2020 majira ya saa kumi na mbili na dakika arobaini jioni, katika kijiji cha isela, kata na tarafa ya Samuye, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga 

“Polisi mkoa wa Shinyanga tulibaini kuwa katika kijiji cha Isela mtoto mwenye umri wa miaka 12 anafunga ndoa ndipo kikosi kazi kutoka dawati la jinsia na watoto Shinyanga wakishirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii halmashauri wilaya ya Shinyanga walifika eneo husika na kukuta sherehe ya harusi ikiendelea nyumbani kwao na bwana harusi na kufanikiwa kuwakamata watu wanne”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Geni Bundala (52), Jumanne Shigimahi (54),Hawa Ramadhan (37) na Japhari Khalfan (52) wote ni wakazi wa kijiji cha Isela. 

“Watuhumiwa hawa tuliwakamata wakimuozesha mtoto (jina linahifadhiwa) , miaka 12, mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Samuye kwa kijana aitwaye Khalfan Japhari,(bwana harusi) mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa kijiji cha Isela ambaye alitoroka na juhudi za kumtafuta zinaendelea”,amefafanua Kamanda Magiligimba. 

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 12 aliozeshwa kwa kutolewa mahari ya ng’ombe 8 na pesa tasilimu laki sita za Kitanzania. 

“Mtoto huyo tayari amekabidhiwa katika kituo cha kulelea watoto ambao ni wahanga wa ukatili -ndoa za utotoni kiitwacho Agape Aids Shinyanga kwa sasa anaendelea na masomo yake”,amesema Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wananchi hususani wazazi na walezi mkoani Shinyanga kuacha kuozesha wanafunzi kwani inapelekea watoto wa kike kukatisha ndoto zao za kuendelea na masomo na hivyo kupelekea kukosa viongozi wanawake wa baadae. 

Aidha amewaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kutokemeza aina zote ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga. 

“Naamini kabisa wananchi wakiendelea kuunganisha nguvu ya pamoja na jeshi la polisi dhidi ya uhalifu, tutaweza kuzuia uhalifu,kupunguza uhalifu na kuufanya mkoa wetu wa shinyanga kuendelea kuwa shwari”,ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527