ALIYEONGOZA KURA ZA MAONI UBUNGE CCM AMPIGANIA BYABATO JIMBO LA BUKOBA MJINI
Na Ashura Jumapili, Bukoba,
Kuwa wa Kwanza kwenye Kura za maoni katika mchakato wa kuwapata wagombea wa Chama Cha Mapinduzi siyo kuteuliwa na muda wa makundi umeisha jambo la msingi ni kumuunga mkono mwenzetu Stephen Byabato.

Hiyo ni kauli ya Almasoud Kalumna ,aliyeongoza Kura za maoni za kuwapata wagombea ubunge Jimbo la Bukoba mjini aliyeongoza kwa kupata kura 116 Kati ya Kura  324 zilizopigwa na wajumbe kwa wagombea  57 waliokuwa wakiwania nafasi hiyo wakati akimnadi mgombea ubunge Jimbo la Bukoba mjini Wakili Stephen Byabato wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi Manispaa ya Bukoba Jumamosi Septemba 5,2020.

Kalumna, alisema watu wote wanajua kuwa aligombea kwenye chama na akaongoza kwenye kura za maoni lakini vikao vyenye kufanya maamuzi viliamua kumteua Stephen Byabato kuwa mgombea ubunge Jimbo la Bukoba mjini kupitia tiketi ya chama Cha mapinduzi ( CCM).

"Umri wangu bado ni mdogo nina kesho nyingi tumpe Byabato Kura za kutosha ili akatuwakilishe vyema bungeni",alisema Kalumna.

Alisema wagombea wote waliokuwa na makundi wayavunje na kujenga nyumba moja .

"Mimi nimezaliwa na kulelewa ndani ya chama Cha mapinduzi hivyo ninakipenda chama changu nitaendelea kukitumikia kwa uwezo wangu wote wa hali na mali",alisema Kalumna.

Pia Kalumna,alimuombea Kura mrithi wa Kata yake ya Ijunganyondo Ally Maghembe na kuahidi katika uzinduzi huo kuwa atakuwa bega kwa bega na mgombea huyo kutafuta Kura.

"Maneno yaliyosemwa na Kalmuna ni maneno yenye busara na yanayotolewa na muungwana"alisema Balozi Khamisi Kagasheki.

Alisema maneno yaliyosemwa na Kalmuna Yana kujenga chama na kukiwezesha kupata ushindi wa kishindo.

Alisema Byabato atafanya kazi na uwezo anao "ninamfahamu vizuri nina ujamaa naye na nimekuja Bukoba kumtafutia kura sababu ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi.

Aliwataka watu wa Bukoba kuachana na mambo yaliyopita ili kuendelea kukijenga chama na kudumisha umoja na mshikamano.

"Ni wajibu wangu kumtafutia Kura mwanasheria maana bungeni wanaenda kutunga sheria ili aweze kuwatumikia wanabukoba",Alisema Balozi Kagasheki.

Kwa upande wake Tobias Mwesiga ,aliyekuwa ameweka nia ya kugombea Jimbo la Nkenge lililopo Wilaya ya Missenyi na kuwa nafasi ya tatu alisema umefika wakati wa Jimbo kurudi CCM.

Mwesiga, alisema ujenzi wa soko na stendi Manispaa ya Bukoba umekuwa ndoto sababu ya kukosa usimamizimakini.

Alisema umoja ndio silaha kubwa ya ushindi katika uchaguzi ni si vinginevyo .

Alisema ,ameongea na mgombea Byabato na kujiridhisha kuwa anatosha kuwa mbunge kwa sababu uwezo na nguvu ya kugombea anayo.

Hata hivyo aliwataka wanaccm kuwa wamoja na kuacha kugawanyika ili kuimarisha nguvu ya pamoja yenye ushindi wa kishindo Jimbo la Bukoba.
Almasoud Kalumna aliyevalia shati la njano akimnadi mgombea ubunge Jimbo la Bukoba mjini Stephen Byabato.
Almasoud Kalumna, akimnadi mgombea udiwani kata ya Ijunganyondo Ally Maghembe.

Kulia ni Balozi Khamisi Kagasheki akimpongeza Almasoud Kalumna
Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527