GGML MDHAMINI MKUU WA MAONYESHO YA TATU YA TEKNOLOJIA ZA UCHIMBAJI MADINI GEITA


 Kushoto ni baadhi ya wafanyakazi wa GGML wakizungumza na wageni wanaotembelea banda la kampuni hiyo lililopo katika maonesho ya teknolojia ya madini mjini Geita
Kulia ni baadhi ya wafanyakazi wa GGML wakizungumza na wageni wanaotembelea banda la kampuni hiyo lililopo katika maonesho ya teknolojia ya madini mjini Geita

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ndiye mdhamini mkuu wa Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia za uchimbaji madini mkoani Geita yatakayofanyika kati ya tarehe 17 hadi 27 Septemba 2020. Mwaka huu, Kampuni ya GGML imetoa udhamini wa kiasi kinachozidi Shilingi Milioni 200 za Kitanzania unaohusisha gharama za kusawazisha eneo la maonyesho pamoja na kugharamia mabanda 100 pamoja na umeme wa dharura (jenereta na mafuta yake) katika kipindi chote cha maonyesho hayo.

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika katika viwanja vya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita ambalo pia limejengwa na Kampuni ya GGML kupitia mpango wake wa huduma kwa jamii kwa gharama za Shilingi Milioni 800.

“GGML inajivunia kudhamini maonyesho haya kwa mwaka wa tatu mfululizo. Mwaka huu tunakusudia kutoa uzoefu wetu wa matumizi ya vifaa mbalimbali vya uchimbaji kwa makampuni mengine lakini pia kwa wachimbaji wadogo. Ni jambo zuri pia kwamba tumetoa udhamini huu tukiwa tunaadhimisha miaka 20 ya uwekezaji wetu mkoani Geita na Tanzania. Tunajivunia kuendeleza ushirikiano na jamii inayotuzunguka kunufaisha wafanyabiashara wa ndani wanaokusudia kufanya kazi na sisi,” alisema Bw Simon Shayo, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu.

Tunafarijika sana kuona ndoto ya kuwa na kituo cha Uwekezaji na biashara ya nje hapa Geita inatimia na GGML inakuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mpango wake wa kusaidia jamii.

Pamoja na tunu yake kuu ya kuisaidia jamii ya Geita kuwa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ambayo yatabakia hata baada ya shughuli za uchimbaji kumalizika, Kampuni ya GGML pia imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Geita ikiwemo uwekezaji wa mradi wa Kituo cha Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita uliotumia bajeti ya Shilingi Milioni 800 za Kitanzania.

Maonyesho haya yatakutanisha kampuni za uchimbaji madini, wachimbaji wadogo na wa kati, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na nchi nyingine kwa ajili ya kuonyesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji madini na fursa za uwekezaji na biashara kwenye sekta hiyo.

Mwaka 2019, Kamati ya Maandalizi ya Maonyesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini, iliitunukia GGML tuzo ya mshindi wa kwanza aliyetoa elimu na mafunzo ya teknolojia muhimu kwa wachimbaji wadogo sanjari na mifumo ya usalama na uokoaji inayopaswa kutumika migodini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527