FACEBOOK YAMZUIA JAMAA ANAYETAKA KURUSHA MATANGAZO MBASHARA 'LIVE' AKIWA ANAKUFA


Facebook imesema itamzuia Mfaransa mmoja ambaye anaugua ugonjwa ambao hauna tiba kurusha moja moja kifo chake kwenye mtandao huo wa kijamii.

Alain Cocq mwenye umri wa miaka 57, amepanga kupeperusha moja kwa moja maisha yake ya siku za mwisho baada ya kuanza kukataa chakula, kunywa chochote na kumeza dawa siku ya Jumamosi.

Rais wa Ufaransa Emmanuela Macron awali alikataa ombi lake la kukatishwa uhai wake.

Bwana Cocq anataka sheria ibadilishwe nchini Ufaransa ili kuruhusu watu walio kwenye maumivu makali kufa kama watakavyopenda.

 Makundi mengine, ikiwemo Kanisa Katoliki,linapinga kukatisha uhai wa mtu kwa mujibu wa maadili ya kanisa hilo.

''Njia ya ukombozi inaanza na niamini , nina furaha,'' Bwana Cocq alichapisha maneno hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook mapema siku ya Jumamosi asubuhi akiwa kitandani nyumbani kwake mjini Dijon baada ya kutangaza kuwa 'amemaliza mlo wake wa mwisho'.

''Ninajua siku kadhaa mbele zitakuwa ngumu lakini nimefanya uamuzi na niko na utulivu,'' aliongeza.

Bwana Cocq ugonjwa ambao umeathiri tishu na viungo, ambao umesababisha kuta za mishipa ya ateri kushikana.

Lakini Facebook imezuia mpango huo wa kurusha moja kwa moja kifo chake, ikisema kuwa hairuhusu kuonesha matukio ya kujitoa uhai.

''Ingawa tunaheshimu uamuzi wa Bwana Cocq kutokana na ushauri wa kitaalamu tumechukua hatua kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya suala la Alain,'' Msemaji wa Facebook ameliambia shirika la habari nchini humo AFP .

''Sheria zetu haziruhusu kuonesha majaribio ya kujikatisha uhai.''
Bwana Cocq alisema Facebook ilikuwa ikizuia matangazo yake mpaka tarehe 8 mwezi Septemba. Amewataka watu wanaomuunga mkono kuishawishi Facebook ibadili msimamo wake.

''Ni juu yenu sasa,'' alisema.

Mwezi Julai, Bwana Cocq aliandika barua kwa Rais Macron, akiomba aruhusiwe kufa ''kwa hiari yake,'' akielezea ''maumivu makali anayoyapata''.

Bwana Macron amesema ''ameguswa'' na barua hiyo, lakini hawezi kumpa ruhusa hiyo kwa kuwa ''hayuko juu ya sheria''.

Suala la kukatisha uhai ni mada tata nchini humo, huku wengi wakiunga mkono haki ya kufa kwa hiari, wakati wengine hasa makundi ya kidini wakipinga suala hilo.
CHANZO - BBC

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527