WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUTUMIA UTAALAMU WAO KWA AJILI YA USTAWI WA TAIFA

Na.Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wauguzi na Wakunga nchini wametakiwa kusimamia na kutoa huduma kwa kuzingatia miongozo iliyopo na kwa kutumia utaalamu wao ili kufikia malengo na matumaini ya wateja kwa weledi mkubwa kwa ajili ya ustawi wa Taifa.


Rai hiyo imetolewa jana  na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu Afya Edward Mbanga wakati wa ufunguzi wa  kikao kazi  cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kinachofanyika jijini hapa.

Bw. Mbanga amesema  kuwa wauguzi na wakunga ndio watendaji wakuu katika vituo vya afya kwenye ngazi ya jamii hadi Taifa hivyo kuwajibika na utawala bora utaboresha utendaji pia kuhakikisha kufikia malengo mbalimbali waliyojiwekea katika ngazi zote.

“Viongozi mnatakiwa kuwa wabunifu, wachapa kazi, wenye nidhamu na mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yenu,kwahiyo  ni lazima msimamie utoaji wa huduma uliyo mzuri na wenye heshima na utu.”Alisema

Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha  washiriki hao kuwa katika huduma za uuguzi na ukunga ni ubinadamu zaidi na kuvaa viatu vya wagonjwa wao “hakuna aliyegongwa muhuri wa kuugua  au kuwa mgonjwa akalazwa ,sisi sote ni wagonjwa watarajiwa kwahiyo kama ambavyo sisi tungependa kuuguzwa vizuri,kijibiwa kwa kauli nzuri basi tuhakikishe tunasimamia maadaili ya kazi”.Alisisitiza Mbanga.

Hatahivyo alisema Serikali inawahakikishia itaendelea kufanya kazi pamoja na waauguzi  kwa kutoa miongozo thabiti na kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo muhimu katika hospitali na vituo vya kutolea huduma ya afya na kuboresha mazingira ya kazi yaliyo bora na salama.

Kwa upande wa malalamiko Kaimu Katibu Mkuu alisema hivi karibuni kumekuwa na malalamko  mbalimbali ya kiutendaji  na kitaaluma kutoka kwa wateja  wanaofika kupata huduma za kiafya na hivyo kuleta taswira mbaya  kwa taaluma yao na kuonyesha hakuna usimamizi mzuri wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga“tungependa  wateja wetu watoe sifa  badala ya malalamiko hivyo kikao hiki mje na mipango ya kuondokana na malalamiko kwani taaluma yenu ni zaidi taaluma.

Kuhusu suala ya rushwa viongozi hao wamekumbushwa kuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa na kuhakikisha inatokomezwa katika maeneo yao ya kazi kwani rushwa imekuwa ikilalamikiwa na kuripotiwa katika kada ya afya nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527