Waliotafuna fedha za Babati Saccos na kuingia mtini,wahitajika Takukuru Manyara Jumatatu.

Na John Walter-Babati
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara inamshikilia Yuda Sendeu kwa tuhuma za kuchukua kisha kukataa kurejesha fedha za Babati Saccos kiasi cha shilingi milioni 44,726,000.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu ameeleza kuwa mwaka 2010, Sendeu alichukua shilingi milioni 35,000,000 kama mkopo ambapo alitakiwa kuzirejesha fedha hizo pamoja na riba ya shilingi milioni 44,726,000 katika kipindi cha miezi 24.

Uchunguzi uliofanywa na Takukuru mkoani hapa unaonyesha kuwa, Sendeu alifanya makubaliano ya kihalifu na baadhi ya wanachama waliochukua fedha katika Saccos hiyo kutokurejesha ili haki za wanachama waaminifu wa Saccos hiyo ziweze kupotea.

Makungu amesema, hadi wanachama waaminifu wa Saccos hiyo ya Babati wanawasilisha malalamiko ya dhuluma hiyo katika ofisi za Takukuru, Sendeu bila kustahili amekaa na fedha hizo kwa miaka kumi sasa.

Makungu ametoa rai kwa wanachama wote wa Babati Saccos ambao wamechukua mkopo na muda wa kurejesha umeshapita, kufika kwa hiari yao ofisi za Takukuru zilizopo mtaa wa Miyomboni mjini Babati siku ya Jumatatu Agosti 10,2020 ili wapewe hesabu zao waweze kurejesha na wale watakaokaidi hatua kali dhidi yao zitachukuliwa kuanzia agosti 12,2020.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post