VIZIWI WAWAOMBA NEC,VYOMBO VYA HABARI, VYAMA VYA SIASA KUTUMIA WAKALIMANI


Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Jamii ya Viziwi nchini imetoa rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Wamiliki wa vyombo vya Habari pamoja na Vyama vya Siasa kuandaa mazingira rafiki ya kuwawezesha kunufaika na taarifa wanazozitoa ikiwemo kutumia wakalimani wa lugha za alama.

Maombi hayo yametolewa leo, Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Nidrosy Mlawa wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria na Kanuni zinazosimamia vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa manufaa ya viziwi nchini.

Mlawa amesema kwamba, vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kutoa habari kwa umma ambapo wapokeaji wa habari hizo wapo katika makundi mbalimbali likiwemo kundi la Viziwi ambalo ni kubwa takribani kila mkoa una viziwi 5000.

“Pamoja na uwepo wa Sheria, Kanuni na miongozo ya utoaji huduma rafiki za habari kwa viziwi bado kuna changamoto nyingi za kiutekelezaji kwa vyombo vya habari nchini, kuelekea uchaguzi mkuu tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wa habari kuhakikisha kuwa viziwi wananufaika na habari za uchaguzi ili wapate haki zao za kupiga na kupigiwa kura”, alisema Mlawa.

Vile vile, Mlawa ameviomba vyombo vya habari kukuza picha ya mkalimani inayoonekana katika televisheni mbalimbali ili waweze kuelewa kwa ufasaha ujumbe unaotolewa pamoja na kuendanisha maandishi na picha halisi wakati wa kutumia maandishi yanayotembea.

Pia, ametoa wito kwa wakalimani wa lugha za alama kuendelea kujisajili Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ili watambulike kisheria na waweze kutoa huduma mbalimbali kwa viziwi nchini.

Kwa upande wake Afisa Jinsia wa CHAVITA, Bi. Lupi Maswanya amesema kuwa kipindi cha kampeni ni kipindi muhimu cha kupata taarifa sahihi ili kufanya maamuzi sahihi ya uchaguzi wa viongozi hivyo wanawakumbusha wamiliki wa vyombo hivyo kuweka wakalimani wa lugha za alama.

“Vyombo vingi vya habari vinalalamikia juu ya gharama kubwa za kuweka wakalimani, kwa kutambua umuhimu wa huduma hii ni vizuri tukakaa pamoja na kuzungumza kufahamu namna ya kufanya juu ya hili”, alisema Bi. Lupi.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kutotumia vibaya lugha za alama na badala yake amewasisitiza kuheshimu lugha hiyo.

Nae, Katibu CHAVITA Mkoa wa Dodoma, Bi Amina Issah ametoa wito kwa wananchi kujifunza lugha ya alama ambapo amesema hivi karibuni kutakuwa na wiki ya viziwi na wamejipanga kuzindua kamusi ya lugha za alama.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post