Usikivu wa TBC Mikoa ya Lindi na Mtwara Waimarika

Na Shamimu Nyaki –WHUSM-Mtwara
Serikali imeendelea kuimarisha usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa TBC kwa idhaa  za TBC Taifa na TBC Fm katika Mikoa ya Lindi na Mtwara  baada ya kufunga Mtambo wenye nguvu ya kilo wati moja (1KW) kwa kila idhaa hizo.

Akizungumza wakati alipotembelea kituo cha kurusha matangazo ya redio hizo cha Lilungu Mkoani Mtwara Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amesema, kuimarika kwa usikivu wa TBC katika  mikoa ya kusini ni jitihada za Serikali kuhakiksha wananchi wake wanapata taarifa ambazo zinaelezea utekelezaji unaofanywa na Serikali kwa ajili ya wananchi wake.

“Wananchi wana haki kikatiba ya kujua Serikali imewafanyia nini,na ili wajue ni kupitia vyombo vya habari vya kuaminika kama TBC,hivyo upanuzi wa usikivu wa shirikia hili umesaidia wananchi kupata habari zinazohusu nchi yao” alisema Dkt.Mwakyembe.

Aidha Dkt.Mwakyembe amesema kuwa kuna changamoto ya miundombinu  ya kufikia maeneo mbalimbali ya mitambo ya TBC hasa barabara kutokana na Mitambo hiyo kusimikwa maeneo ya miinuko,ambapo ameahidi kuwasiliana na Mamlaka husika ziweze kushughulikia changamoto hiyo.

Kwa upande wake Mhandisi wa Shirika hilo Bibi.Upendo Mbele amesema kuwa fedha za maendeleo zilizotengwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya usikivu zimesaidia kuboresha mradi wa Kilwa na Ruagwa ambao utasaidia katika kuongeza nguvu ya usikivu.

“Kituo hiki cha Mtwara kimepatikana kutokana na juhudi na mipango ya shirika kutumia mafundi wa ndani na  vipuri vya vituo  vya Namanga,Rombo,Tarime,Kibondo na Mbamba Bay ambavyo vilitumika kuunda mtambo huu”alisema Bibi Upendo.

Naye Fundi Mitambo wa Shirika hilo Bw.Hamis Kalanje amesema kuwa kituo hicho kimeanza kurusha matangazo kwa mitambo ya FM kwa idhaa za TBC TAIFA kwa masafa ya 87.7Mhz na TBC FM kwa masafa ya 89.7Mhz kwa uwiano wa nguvu ya kilo wati moja kwa kila mtambo.

“Baada ya kufunga mtambo huu usikivu umeongezeka katika maeneo ya Msimbati, Mtendachi,Kilambo,Mayanga,Mikindani,Nanguruwe,Mpapura  na  Ndumbwe”alisema Bw.Kalanje.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amezindua kituo cha redio cha Hopaje FM (Nyakati za Kusisimua) kilichopo Mtwara ambapo amewahimiza wanahabari wa kituo hicho kufanya kazi kwa weledi na kufuata miiko ya taaluma ya habari,ambapo pia amesisitiza kutoa habari zinazoelezea utekelezaji wa serikali kwa wananchi wake na kusisitiza amani katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

…MWISHO..


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post