SIMBACHAWENE AVIONYA VYAMA VYA SIASA VITAKAVYOLETA VURUGU WAKATI WA UCHAGUZI MKUU

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Kigoma.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amevionya nyama vya siasa nchini ambavyo vina wanawagombea katika ngazi mbalimbali vizingatie sheria kwa kuhakikisha wanachokifanya hakileti uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Pia amelitaka Jeshi la Polisi nchini kusimamia amani na utulivu, kuanzia Polisi Kata, Wilaya mpaka Mkoa kuwathibiti watu watakaoleta fujo na wasisubiri mpaka Kamishna Jenerali wa Polisi aseme.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kigoma, kabla ya kuanza ziara katika makambi ya Wakimbizi Mkoani humo, Simbachawene alisema mtu yeyote, chama chochote kitakacholeta vurugu lazima adhibitiwe.

“Lazima sheria ifuatwe, hatufanyi uchaguzi kama sisi ni wanafunzi wa uchaguzi, sisi watanzania katika ukanda huu tumefanya uchaguzi wa demokrasia mara nyingi kuliko nchi yoyote, haiwezekani tukasikia watu bado wanakufa kwenye harakati za uchaguzi, nchi hii inamaana zaidi kuliko hiyo unayoifikiria siasa,” alisema Simbachawene.

Aidha, Simbachawene alisema Tanzania ina wakimbizi zaidi ya 288,000, idadi hiyo ni kubwa sana ambayo ni sawa na wingi wa wilaya mojawapo nchini.

“Idadi hiyo ni wageni ambao wapo kwenye makazi na pia katika makambi, wapo wengine tulishawapa uraia, lakini wapo humu humu, wapo wengine wanaenda kwao na kurudi kwasababu tunanjia ya mpaka ipo wazi, katika hili lazima tuweke mikakati madhubuti sana kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi, Shirika la UNHCR ili tuweze kuwarudisha wakimbizi hawa ambao kwao sasa kuna amani na wamefanya uchaguzi wa amani na wamepata kiongozi wao,” alisema Simbachawene.

Alisema inataka Wakimbizi warudi kwao kwa hiari na idadi ya 400 kwa wiki wanaorudishwa Burundi ni ndogo hivyo Serikali itaweka mchakato ili kufanikisha wakimbizi wanarushwa kwa wingi nchini kwao.

Pia Waziri Simbachawene alizungumzia changamoto ya upatikanani wa Vitambulisho vya Taifa hasa katika Mkoa wa Kigoma uliopo mpakani ambapo aliviomba vyombo vya ulinzi vishirikiane katika mchakato wa kupata vitambulisho kwa wakazi wa Mkoa huo.

“Mchakato wa kupata kupata kitambulisho cha Uraia ni mchakato mkubwa sana, rai yangu mngetengeneza kikosi kazi cha Mkoa kwa kusaidiana na Uhamiaji ili waweze kufanya upekuzi na waweze kutoa huo utambulisho na hatimaye NIDA waweze kutoa kitambulisho kwa muhusika anayeomba kitambulisho,” alisema Simbachawene.

Waziri Simchawene, Jumatatu Agosti 17 anaendelea na ziara yake kwa kutembelea kambi za wakimbizi za Nyarugusu Wilayani Kasulu, na Nduta iliyopo Wilaya ya Kibondo na Kambi ya Mtendeli iliyopo Wilaya ya Kakonko Mkoani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post