SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 15.2 KUTOKA NMB

 Na. Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Serikali  imepokea gawio la kiasi cha shilingi bilioni 15.2 kutoka Benki ya NMB, ikiwa ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 48 iliyopatikana katika benki hiyo kwa Mwaka wa fedha 2019/2020.

Makabidhiano ya mfano wa hundi za gawio hilo yalifanyika jijini Dodoma kati ya Mweyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Dkt. Edwin Mhede na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Isidor Mpango, aliyepokea gawio hilo kwa niaba ya Serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mpango, alisema Serikali inathamini mchango wa Benki ya NMB katika maendeleo ya nchi na kuupongeza uongozi wa benki hiyo kwa jitihada mbalimbali za kuchaingia uchumi wa nchi ikiwemo kutoa gawio ambalo mwaka huu limeongezeka.

Katika mwaka wa Fedha 2018/19, Benki ya NMB ilitoa gawio la shilingi bilioni 10.48 na mwaka huu imetoa shilingi bilioni 15.2, sawa na ongezeko la asilimia 45.

“Ni mafaniko makubwa kwani faida imepatikana wakati wa changamoto ya ugonjwa wa Covid 19, NMB ni ya nfano katika sekta ya fedha hapa nchini,” alisema Dkt. Mpango.

Waziri Mpango alifafanua kuwa Wizara yake itahakikisha fedha hizo zinatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutatua baadhi ya kero za wananchi na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Aidha Waziri Mpango ameiagiza benki ya NMB Pamoja na taasisi nyingine za fedha nchini kutumia utaalamu kutafuta suluhisho la riba kubwa ili amana na mikopo kwa wananchi iongezeke.

“Benki zijitahidi kujua uchumi wa maeneo mbalimbali na kuandaa namna ya kuwafikia wateja katika maeneo yao ya biashara, kuwapatia elimu ya fedha na kusimamia vizuri kanuni za utoaji mikopo,” alisisitiza Dkt. Mpango.

Alizitaka benki na taasisi zote za fedha nchini kushughulikia mikopo chechefu ili uwiano wa mikopo yote isivuke asilimia tano na kuhakikisha wananchi hususan wakulima na wananchi wa chini waweze kufikiwa.

Aidha, Dkt. Mpango alimpongeza Msajilli wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka kwa usimamizi wa mashirika ya umma, taasisi Pamoja na kampuni na kuwezesha Serikali kupata gawio kulingana na uwekezaji.

Waziri Mpango amewapongeza wanahisa wengine wa benki ya NMB hasa Rabo Bank kwa kuwa wabia wazuri na kuwa Serikali inathamini mchango wao katika maendeleo ya benki ya NMB na itaendelea kushirikiana nao.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka alifafanua kuwa mchango wa mashirika ya umma, taasisi pamoja na kampuni umeongezeka ambapo gawio la Serikali limeongezeka ambapo mwaka 2014/15 Serikali ilipata gawio la Sh. bilioni 161 hadi kufikia Sh. trilioni 1.05 mwaka wa fedha 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 521” Alisema Bw. Mbuttuka.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede aliahidi kuwa benki hiyo inatarajia kuongeza kiwango cha gawio kwa Serikali katika mwaka ujao wa fedha 2020/21 baada ya Benki hiyo kupata faida ya shilingi bilioni 93.6 katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna, alisema kuwa gawio la shilingi bilioni 15.2 linatokana na uwekezaji wa Serikali wa asilimia 31.8 za hisa katika benki hiyo.

Alisema pamoja na kutoa gawio kwa Serikali benki hiyo imekuwa ikishiriki katika miradi mbalimbali ya kimkakati ya Taifa ikiwemo kutoa dhamana katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), mradi wa Umeme Kinyerezi II Pamoja na kuchangia huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, afya na kilimo na kuahidi kuwa benki hiyo itaendelea kutoa mchango chanya katika jamii.

Bi.  Zaipuna alinainisha kuwa pamoja na kutoa gawi hilo, Benki yake pia imelipa kodi mbalimbali serikalini zikiwemo kodi ya mapato, kodi ya maendeleo ya ujuzi, ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani zenye thamani ya shilingi bilioni 170.8

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527