MAKALA - HESLB WALIVYOFAFANUA HOJA NA MASWALI YA WAOMBAJI MIKOPO WA ELIMU YA JUU MIKOA YA KIGOMA NA GEITA

Na Ismail Ngayonga-HESLB

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) hivi karibuni imefungua dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa  masomo 2020/2021.


Kufunguliwa kwa dirisha hilo kunatoa fursa kwa Wanafunzi mbalimbali waliohitimu masomo ya kidato cha sita na ngazi ya stashahada kutoka katika vyuo mbalimbali nchini kutuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwezeshwa na serikali katika gharama za ada, chakula na malazi pindi wawapo masomoni.

Katika kuhakikisha kuwa kila wanafunzi wote wa Kitanzania wenye sifa stahiki wananufaika na mikopo hiyo, HESLB imetoa mwongozo wa uombaji wa mikopo unaoanisha hatua muhimu na za msingi zinazopaswa kuzingatiwa na waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021.

Itakumbukwa kuwa katika kila mwaka wa masomo pindi unapotaraji kuanza, Serikali kupitia HESLB imekuwa ikitoa mwongozo kwa waombaji mikopo, ikiwa ni mojawapo ya hatua mahsusi iliyolenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanufaika wanapata fursa ya kufahamu vigezo na sifa mbalimbali vinavyotumika katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Aidha pamoja na kutoa miongozo hiyo, utafiti uliofanywa na HESLB umebaini kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa kupata mikopo ya elimu ya juu kutokana na kufanya makosa mbalimbali wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo kama inavyoelekezwa katika mwongozo wa mwaka husika.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia HESLB kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020 imekuwa ikiendesha programu mafunzo ya elimu kwa umma kwa wanafunzi wanaotaraji kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa kutembelea mikoa mbalimbali nchini ili kutoa ufafanuzi na hatua mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa katika kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru anasema katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga fedha za mkopo kiasi cha Tsh. Bilioni 464 zinazotarajia kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000 wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo.

Anaongeza kuwa bajeti ya Tsh. Bilioni 464 kwa mwaka 2020/2021 imeongezeka kutoka Tsh. Bilioni 450 mwaka 2019/2020 ambazo ziliwanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119, ambapo  ongezeko hilo la bajeti inatokana na adhma ya serikali ya kupanua wigo wa elimu ya juu hususani kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi.

Hivi karibuni HESLB iliendesha mafunzo ya programu ya elimu kwa umma katika mikoa 14 nchini yakiwa na lengo la kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali kutoa kwa wadau wa elimu nchini ikiwemo wanafunzi, watendaji wa serikali na watoa huduma za mtandao katika ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini.

Mikoa hiyo ni pamoja na Rukwa, Mbeya, Katavi, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Geita, Kigoma pamoja na Zanzibar Unguja (Mjini Magharibi, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Pemba Kaskazini, Pemba Kusini), ambapo Maofisa Mikopo wa HESLB waliweza kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wakati wa uombaji wa mikopo ya elimu ya juu unaofanyika kwa njia ya mtandao.

Wakati wa mafunzo hayo, katika Mikoa ya Geita na Kigoma Maofisa wa HESLB waliweza kufanya jumla ya mikutano 7 katika Halmashauri za Wilaya ya Geita, Chato, Bukombe, Mbogwe (Mkoa wa Geita) pamoja na Wilaya za Kasulu, Kibondo na Manispaa ya Kigoma Ujiji (Mkoa wa Kigoma) ambapo waliweza kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali 159 kutoka kwa wanafunzi 3500 waliohitimu kidato cha sita na masomo ya stashahada katika Mikoa hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Mkoani Geita, Meneja Mikopo wa HESLB Kanda ya Ziwa, Usama Choka anasema pamoja na nia njema iliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini wananufaika na mikopo hiyo, bado miongoni mwao wamejikuta wakikosa fursa hiyo kutokana na kufanya mbalimbali wakati wa kujaza fomu za maombi.

Anaongeza kuwa utafiti uliofanywa na HESLB umebaini kuwa wanafunzi wengi hususani wanaotoka katika kaya maskini wamejikuta wakikosa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kutokana na kukiuka maelekezo yanayotolewa katika mwongozo wakati wa kujaza fomu za maombi mtandaoni.

‘’Wanafunzi wengi wanaotoka katika kaya maskini hususani waliopo katika Mikoa ya pembezoni, wamekuwa wakishindwa kukamilisha baadhi ya maelekezo yanayotolewa wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu kupitia mtandao, hivyo HESLB tumeamua kuanzisha programu ya elimu ya mafunzo ya jinsi ya kujaza fomu hizo ili kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo hii’’ alisema Choka.

Aidha Choka anazitaja baadhi ya changamoto ni pamoja na waombaji wengi kusahau kupiga mihuri fomu, uwekaji wa saini ya mwombaji pamoja na mdhamini pamoja na kuacha kudhibiti cheti cha kuzaliwa katika mamlaka za serikali ikiwemo Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufulisi (RITA), na hivyo kufanya maombi yao kutofanyiwa kazi wakati wa zoezi la upangaji wa mikopo.

Kwa mujibu wa Choka anasema kutokana na kutambua ukubwa wa tatizo hilo, pamoja na kuendesha kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu nchini, HESLB pia imefungua Ofisi za Kanda katika Mikoa 6 nchini ikiwemo Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza, Mtwara pamoja na Zanzibar.

‘’Tumefungua ofisi kwa malengo mahsusi ya kusaidia waombaji wa mikopo hii ambao idadi yao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku, kujaza fomu zao kwa usahihi pamoja na kuwasaidia pale wanapopata changamoto mbalimbali wakati wa kuwasilisha kudhibitisha nyaraka zao katika mamlaka mbalimbali za Serikali’’.

Akifafanua zaidi, Choka anasema HESLB pamoja na kutoa mwongozo kwa waombaji wa mikopo hiyo, katika mwaka huu wa masomo 2020/2021 HESLB pia imetoa mwongozo kwa watoa huduma za mtandao (internet) unaoanisha hatua mbalimbali muhimu zinazopaswa kuzingatiwa na watoa huduma za mtandao kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Kwa upande wake, Afisa Mikopo wa HESLB Jonathan Nkwabi aliwataka wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo kwa mwaka 2020/2021 kujihadhari na kundi la matapeli ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwadanganya kuwa ni mawakala waliotumwa na Ofisi hiyo huku wakidai kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wakati wa kutuma maombi yao.

‘’Uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi kunaibuka wimbi la matapeli wanaoanzisha makundi ya mtandaoni ikiwemo whatsapp na kuanza kuwadai kuchangisha pesa ili kuwasaidia kujaza fomu, ukweli ni kuwa HESLB haina wakala yoyote hivyo watu hao ni matapeli, tunawashauri kusoma mwongozo wetu na iwapo kutatokea changamoto zozote pigeni simu zetu zilizotolewa katika mwongozo wa maombi’’ alisema Nkwabi.

Nkwabi anasema Serikali imetoa kipaumbele cha mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wote hususani wanaotoka katika kaya maskini na kusisitiza kuwa hakuna upendeleo unaotumika wakati wa upangaji mikopo hiyo na badala yake wanafunzi wahitaji wanatakiwa kujaza fomu kwa usahihi na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ikiwemo vyeti vya vifo iwapo mwombaji amepoteza mzazi/wazazi.

Akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo, Grace Selestine ambaye ni mhitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Udizungwa iliyopo Mkoani Iringa ameipongeza Serikali kupitia HESLB kwa kutoa mikopo ya elimu ya juu nchini kwani imekuwa faraja kubwa kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini.

Anasema utaratibu wa utoaji mikopo ni mzuri kwa kuwa unaongeza fursa na wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu kwa usawa pasipo na ubaguzi, kwani silaha ya kujikwamua na umaskini wa fikra na kipato katika ngazi ya kaya ni pamoja na uhakika wa elimu bora.

‘’Tunaoipongeza HESLB kwa kuweka utaratibu wa mafunzo elekezi kuhusu namna ya kujaza fomu za maombi ya mikopo tunaomba utaratibu huu uwe endelevu ili uweze kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu hususani kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini’’ alisema Grace.

Naye Erick Bukuru, mhitimu wa Kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Ilboru Mkoani Arusha alisema mafunzo ya mwongozo wa uombaji mikopo yamewasaidia kupata ufafanuzi kuhusu vigezo na sifa zinazotumika katika upangaji wa kiwango cha mikopo baina ya mwombaji mmoja na mwingine kwani awali suala hilo lilikuwa likiwachanganya wanafunzi wengi.

Bukuru aliipongeza HESLB kwa kutoa mwongozo wa uombaji mikopo katika kila mwaka wa masomo, kwani umewawezesha waombaji wengi kufahamu kipaumbele kinachopangwa na Serikali katika uhitaji wa mikopo ya elimu ya juu na utofauti uliopo baina ya mwombaji mmoja na mwingine na kutokana na sifa na vigezo vilivyoanishwa.

Aidha Jeremiah Deus mhitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Umbwe iliyopo Mkoani Kilimanjaro alisema mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na HESLB tangu mwaka 2005 imekuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi yaliyofikiwa na Tanzania ikiwemo kufikia nchi ya kipato cha kati kabla ya muda wa malengo yaliyowekwa katika dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025.

‘’Elimu ndio mhimili wa maendeleo ya nchi, kupitia mikopo ya elimu inayotolewa na HESLB imesaidia kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali za kiuchumi, na kuwa chachu ya kufikia nchi ya kipato cha kati, nashauri kila mwaka Serikali iendelee kuongeza bajeti ili Wanafunzi wengi hususani wanaotoka katika familia za kaya maskini waweze kunufaika’’ alisema Jeremiah.

Programu ya mafunzo ya elimu kwa umma kupitia kampeni ya WeweNdoFuture iliyoanza kutolewa na HESLB hivi karibuni kuhusu taratibu za uombaji mikopo wa wanafunzi wa elimu ya juu nchini, ni mojawapo ya mikakati inayotumika katika kuhakikisha kuwa wanafunzi waombaji wanajaza fomu zao kwa usahihi ili kuepuka makosa yanayoweza kuwakosesha sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu.

Kupitia utaratibu huo, HESLB imefanikiwa kufanya mikutano na kutembelea wadau wake mbalimbali ikiwemo wanafunzi, watoa huduma za mtandao (internet) pamoja na watendaji wa mamlaka za mitaa ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sifa na vigezo vinavyotumika katika upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

MWISHO.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post