Bilioni 15 Zatumika Kukopesha Pembejeo Kwa Wakulima-Kusaya

Serikali ya Awamu ya Tano imetumia shilingi Bilioni 15 kwa ajili mikopo ya pembejeo kwa wakulima tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015.

Kauli hiyo imetolewa jana (08.08.2020) na Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane Nyakabindi mkoani Simiyu wakati akikabidhi matrekta mawili kwa wakulima wa wilaya Meatu 


“ Rais Dkt.John Pombe Magufuli amekwisha toa zaidi ya shilingi Bilioni 15 kwa ajili ya mikopo ya pembejeo kwa wakulima tangu alipoingia madarakani iliyosaidia kukuza sekta ya kilimo kwa kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo” alisema Kusaya


Kusaya aliongeza kusema kuwa Wizara ya Kilimo kupitia Mfuko wa Pembejeo (AGITF) umekwisha toa jumla ya mikopo 314 wakulima na kuchangia upatikanaji wa ajira 364 kwenye viwanda vitatu vya kuchakata mbegu za mafuta nchini.


Katika hafla hiyo, wakulima wawili Juma Mpina toka Kisesa Magu na Pius Machungwa toka Meatu walikabidhiwa matrekta mawili kila moja likiwa na thamani ya shilingi milioni 60 ikiwa ni mkopo toka AGITF.


“Leo nimekabidhi matrekta mawili kwa wakulima hawa, nitumie fursa hii kuwahamasisha wakulima kuja Wizara ya Kilimo kupata mikopo kwa mtu mmoja moja au kikundi kwa riba ya kati ya asilimia 6 hadi 7 katika kipindi cha miaka miwili” alisisitiza Katibu Mkuu.


Mfuko wa Pembejeo hutoa asilimia 90 ya fedha zinazohitajika  kwenye mkopo wa trekta na mkulima anatoa asilimia 10 inayotakiwa ambapo lengo la serikali ni kuwezesha wakulima wengi kupata pembejeo bora na zenye gharama nafuu ili kukuza uzalishaji wa mazao ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi.


Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post