TENKI LA LORI LA MAFUTA LACHOMOKA NA KUZUA TAHARUKI KAHAMA MJINI..LAJERUHI NA KUHARIBU MALI


Muonekano wa tanki la mafuta baada ya mfuniko wake kuripuka gari likitengenezwa Kahama Mjini.


Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog Kahama
Taharuki ya aina yake imetokea Mjini Kahama baada ya mfuniko wa tanki la mafuta lenye namba za usajili T340 BEZ likiwa kwenye gari lenye namba za usajili T393 BEZ aina ya IVECO kuchomoka wakati likifanyiwa matengenezo katika eneo la Bijampola wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea leo Jumapili Agosti 9,2020 majira ya saa tatu na nusu asubuhi wakati lori hilo likichomelewa sehemu ya kuweka Fire Extinguisher ambapo ghafla sehemu ya nyuma ya kuwekea mafuta ililipuka na kutoka kwenye gari hilo na kusababisha majeruhi kwa watu wawili na kuharibu paa ya nyumba moja.

"Baada ya sehemu hiyo ya nyuma ya kuwekea mafuta kulipuka ghafla ilisababisha majeruhi kwa watu wawili ambao ni Bahati William ambaye amevunjika mkono wa kulia na mwingine ni Zainab Said ambaye amejeruhiwa mkono wa kushoto baada ya kuangukiwa na sehemu hiyo ya tanki la mafuta iliyochomoka",amesema Kamanda Magiligimba.

Aidha ameeleza kuwa kipande kingine  cha bati la tanki la mafuta kiliruka na kusababisha uharibifu wa paa la nyumba ya Amour Hamad na thamani ya uharibifu haijajulikana.

"Chanzo cha tukio hilo ni kuchomelea tanki la mafuta bila kuchukua tahadhari na kuzingatia masharti ya ufundi wa gari lenye tenki la mafuta",amesema Kamanda Magiligimba.

Amesema dereva wa gari hilo amekamatwa na fundi aliyekuwa anachomelea gari hilo amekimbia na kwamba majeruhi wamepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama kwa ajili ya matibabu.

Mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Dk Lucas David amethibitisha kupokea majeruhi mmoja ambaye ametokana na ajali ya kulipuka kwa tanki la Mafuta iliyotokea leo katika eneo la Bijampola ambaye amepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake na anaendelea kupatiwa matibabu.

Akizungumza na Malunde 1 blog,mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Baraka John amesema kuwa akiwa katika eneo lake la kazi majira ya saa tatu asubuhi leo Jumapili Agosti 9,2020 wakati mafundi wa kuchomelea magari wakiwa wanalifanyia matengenezo gari hilo ghafla lililipuka na kusababisha madhara mbalimbali.

Amesema mafundi waliokuwa wanatengeneza gari hilo hawakuchukua tahadhari ili kujiridhisha kama kuna mafuta yaliyosalia kabla ya kuanza kulichomelea hali iliyosababisha kujitokeza kwa mlipuko huo ambao umesababisha majeruhi mmoja na kuharibu mali mbalimbali katika eneo hilo ikiwemo vibanda na nyumba.

“Magari kama haya yanayobeba vimiminika vinavyolipuka ni bora yakazuiwa kufanyiwa matengenezo katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu au kwenye makazi ya watu,serikali ipige marufuku uchomeleaji wa magari haya mitaani kwani ni hatari kwa usalama,”amesema John.

Naye Joyce Paulo anayejihusisha na shughuli ya kuuza vyakula 'Mamalishe' katika eneo la Bijampola amesema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwani mlipuko huo ulikuwa ni mkubwa na baadhi ya vyuma vilikuwa vinaruka katika maeneo mbalimbali huku moshi mkubwa ukiwa unasambaa kwa kasi katika makazi ya watu.

“Tulidhani ni bomu limelipuka katika eneo letu kwani nyumba ya jirani yetu imeharibiwa sana na baadhi ya vyuma vilivyokuwa vinajitokeza baada ya kulipuka,tunaiomba serikali idhibiti uegeshaji ovyo wa magari yenye mafuta katika eneo hili,”amesema Joyce.
Muonekano wa tanki la mafuta baada ya mfuniko wake kuripuka gari likitengenezwa
Nyumba ikiwa imeharibika baada ya mfuko wa tanki la mafuta kuripuka gari likitengenezwa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post