WIZARA YA KILIMO YAJIPANGA KUKUZA KILIMO CHA MBOGA MBOGA NCHINI


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya leo (tarehe 20/07/2020 ) amesaini mkataba wa makubaliano kati ya Wizara ya Kilimo na World Vegetable Center ili kuboresha utafiti na uendelezaji wa mazao ya mboga mboga ili kusaidia kuboresha lishe na kuongeza usalama wa chakula.


Mkataba wa makubaliano umesainiwa Jijini kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kwa niaba ya serikali na Dkt.Gabriel Rugalema Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini (avrd-World Vegetable Center) 


 Makubaliano hayo yapo katika maeneo makuu matatu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji, uchakataji na utunzaji wa mbegu za mazao ya mboga mboga kwa ajili ya matumizi ya kisayansi kwa sasa na vizazi vijavyo,


 Eneo la pili la makubaliano ni utafiti wa mbegu bora zenye kuhimili ukinzani wa magonjwa, wadudu, na hali ya hewa kama vile ukame, mafuriko na mabadiliko ya tabia nchi kwa ujumla na tatu kujenga weledi wa wana sayansi, maafisa ugani kilimo, wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya kilimo na wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo, teknolojia mpya na kilimo biashara kufuatana na matakwa ya Serikali na wadau wengine.


Aidha, Kusaya amesema kuwa makubaliano ya ushirikiano huu ni mwendelezo wa makubaliano ya ushirikiano kati ya serikali kupitia Wizara ya Kilimo na AVRDC- World Vegetable Center iliyoanza mwaka 1992 ambapo kwa wakati huo Serikali ilikubali kuanzisha kituo cha utafiti wa mboga mboga Tengeru mkoani Arusha kwa niaba ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC).


“Kupitia makubaliano haya,tutaweza kutumia fursa hii kuimarisha utafiti wa mazao ya mboga mboga na kuongeza ujuzi na weledi wa wataalam wetu ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa vyuo vyetu vya kilimo ili sekta ya mboga mboga ichangie ipasavyo katika uongezaji tija na kuchangia pato la Taifa” alisema Kusaya


Kusaya amesema Wizara yake ina vyuo vya mafunzo ya Kilimo 14,taasisi za utafiti wa Kilimo 17 na vituo mahususi 18 ambavyo kupitia ushirikianao huu vitaweza kutumika kuzalisha mbegu bora za mazao ya horticulture na kuwafikia wakulima kote nchini.


Hata hivyo Kusaya ametoa wito kwa wakurugenzi wa Wizara ya Kilimo kusimamia yale yaliyoko kwenye mkataba na kuhakikisha yanatekelezwa ipasavyo. 


“Ili hili lifanyike ningependa kuwepo kamati ndogo ndogo hapa Wizarani itakayofuatilia utekelezaji wa makubaliano haya na makubaliano mingine ya aina hii, ninawataka idara zinazohusika  kushirikiana na TARI na TPRI kuandaa mpango kazi wa utekelezaji” alisema Katibu Mkuu Kusaya


Naye Mkurugenzi wa World Vegetable Center Dr. Gabriel Rugalema amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1997 hadi 2018 wameweza kuzalisha aina 18 za mbegu bora za mazao tofauti ( nyanya,ngogwe,mchicha,mnafu,figiri au loshuu)


“ Mbegu za nyanya tu zinakadiriwa kuchangia Dola za Kimarekani  milioni 250 katika uchumi wa Tanzania kwa miaka mitano iliyopita pamoja na kuongeza ajira na pato la familia” alisema Dkt.Rugalema.


Aliongeza kusema jumla ya wataalam 400 kutoka nje ya nchi waliopata mafunzo kati ya mwaka 1998 na 2018 na wataalam zaidi ya 2000 kutoka ndani ya nchi wamepatiwa mafunzo kati ya mwaka 1994 hadi sasa.


AVRDC kupitia kituo chake cha World Vegetable Center kilichopo Tengeru Arusha kimefanikiwa pia kufundisha zaidi ya wakulima 200,000 Tanzania Bara na Visiwani elimu juu ya mazao ya mboga mboga ili kuinua uzalishaji wake na kuongeza kipato cha wakulima.


Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527