WIZARA YA ELIMU NCHINI KENYA YAFUTA KALENDA YA MASOMO KWA SHULE ZA UPILI NA MSINGI KWA MWAKA 2020 KISA CORONA


Wizara ya elimu nchini Kenya imefuta Kalenda ya masomo kwa shule za upili na msingi kwa mwaka 2020.



Waziri wa elimu nchini Kenya Prof. George Magoha ametangaza kuwa hakutakuwa na mitihani ya kitaifa ya mwaka huu ya darasa la nane (KCPE) na kidato cha nne (KCSE).



Magoha amesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya misururu ya mikutano ya ushauriano na washikadau wakiwemo walimu, wazazi na watalaam wa afya.

Kutokana na uamuzi huo, mitihani ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) itaandaliwa mwaka 2021.

"Mwaka wa 2020 umeharibiwa na COVID-19 hivyo wanafunzi wa msingi na upili watarudia madarasa 2021. Mitihani ya kitaifa itaandaliwa baadaye 2021," amesema Magoha.

Waziri huyo amesema uamuzi huo wa kufungua shule mwaka 2021 ulichochewa na kuongezeka kwa idadi ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Magoha pia amedai kuwa wizara hiyo ilitambua kuwa kutekeleza sheria ya kukaa mbali na masharti mengine huenda ikawa changamoto katika shule za msingi na upili kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.

"Tuliamua kuahirisha kufunguliwa kwa shule hadi Januari 2021 kwa sababu tuna imani kufikia wakati huo makali yatapoa na idadi kupungua na pia tutakuwa tumejifunza mengi kuhusu virusi hivyo," amesema Magoha.

Taasisi za Mafunzo ya Ufundi (TVETs) zimeshauriwa kujiandaa kufungua mnamo Septemba chini ya masharti makali yanayoafikiana na maagizo ya Wizara ya Afya.

Vyuo vikuu navyo vitafunguliwa kwa hatua na wizara hiyo itafanya zoezi la kubaini taasisi ambazo zimetimiza mahitaji yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527