ALIYEKUWA MBUNGE RORYA AJIUZULU KUGOMBEA UBUNGE BAADA YA KUREJESHA FOMU... 'MIMI DARASA LA 7 NAWAACHIA WASOMI"


Kulia ni Lameck Airo akirudisha fomu kugombea Ubunge jimbo la Rorya kupitia CCM kabla ya kujiuzulu kugombea


Na Dinna Maningo - Malunde 1 blog Rorya.
Mbunge wa Jimbo la Rorya aliyemaliza muda wake Lameck Airo  ambaye alichukua fomu kutetea nafasi yake ya Ubunge amejiuzulu kuomba  kugombea ubunge kwa kile alichoeleza kuwa ameamua kuwaachia wasomi  na kuunganisha nguvu ya pamoja kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinapata ushindi mnono zaidi.

Mnamo Julai 17,2020 Airo alichukua fomu ya kutia nia ya Ubunge na kuirejesha na kufikisha idadi ya Watia nia 49 lakini jana Julai 18,2020 alikabidhi barua mbele ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) wilaya ya Rorya Avelin Ngwada ,Kamati ya Siasa ya Wilaya na Watia nia nafasi ya Ubunge.

"Nimeahirisha kwa roho moja sijashinikizwa  na mtu nimewaachia na wengine waendelee atakayeshinda nitamuunga mkono kwa maslahi ya Rorya kwa hiyo watu wasiwe na shaka",alisema Airo.

Alivyohojiwa na Malunde 1 blog kutaka kufahamu kwanini ameahirisha kugombea licha ya kwamba alichukua fomu ya kugombea kwa hiari alisema : 

"Nilikuwa tu natesti mitambo maana nilishawahaidi wananchi kwenye mikutano yangu kuwa sitogombea napumzika lakini cha hajabu baadhi ya wana Rorya wakiwemo wasomi wakawa wananitukana kwenye mitandao ya kijamii mara mimi ni darasa la saba naongozaje na wasomi  nimevumilia mengi sana na hao waliokuwa wananitukana baadhi yao ni wasaliti wa chama na leo wametia nia kugombea" .

"Nilipoona wananiandama nikasema acha nichukue fomu tujipime na hao wasomi, waliposikia nimechukua fomu wakaanza tena kupata presha kulalamika lakini nimetafakari zaidi nikaona kwanini tusumbuane  na Rorya ni yetu sote ndipo nikaamua kuahirisha ili na wasomi nao waongoze wananchi wapime,nimezaliwa Rorya hivyo naahidi kutoa ushirikiano",alisema Airo.

Airo alisisitiza kuwa atakayefanikiwa kuwa Mbunge asiishie kukaa mjini afike Jimboni ashiriki maendeleo kulinganana na uwezo wake hata kama kipato chake ni kidogo lakini msaada wake utasaidia kulingana na uwezo wake.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Rorya Charles Ochele aliwashukuru Wananchi wa Rorya kwa kuwathamini watu wa elimu ya darasa la saba nakuwapa ridhaa katika nafasi mbalimbali ndani ya chama na Ubunge na nafasi zinginezo

"Airo kaongoza sasa tunarudisha wasomi,sababu ya kuchukua darasa la saba  tulikuwa tunawapa wasomi lakini wanaishia kukaa Dar es Salaam Jimboni anarudi kwa nadra tukasema hatuchagui mtu wa Dar lakini sasa tumeamua kuwapa wasomi ili tuone kama wamebadilika na tuwapime kwa vitendo wasipoleta mabadiliko tutaendelea na msimamo wakuwakataa wagombea wanaotoka Dar ",alisema Ochele.

Ochelle aliwaonya wanachama wanao mchafua Airo na Mwenyekiti huyo kwenye mitandao ya kijamii na badala yake waungane pamoja kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza katika Jimbo hilo huku akikemea vitendo vya rushwa kwa watia nia.

Kitendo cha Airo kujiuzulu kugombea kimewafurahisha Watia nia ambao wamedai kuwa walipata hofu baada ya kuona amechukua fomu na baadhi yao hawakupata usingizi lakini sasa hofu imetoweka.

Mtia nia nafasi ya Ubunge Maina Owino alisema : "Kwa kweli mbunge umetusumbua moyoni mwetu umetupa presha sana niliposikia umechukua fomu sikupata usingizi lakini tunashukuru umeachia sasa tutakuwa huru".

Peter Sarungi alimuahidi Airo kuendelea kufauta nyayo zake,busara zake na ushirikiano kwa kuwa wote ni wana Rorya lakini pia alimpongeza yeye  na Ochele kwa kuwasamehe wale waliokuwa wakiwachafua kwenye mitandao ya kijamii na kuahidi kufungua ukurasa mpya ili kuhakikisha Rorya inasonga mbele.

Ngwada alisema kuwa baada ya Airo kujiondoa  wamebaki 48 ambapo waliochukua fomu walikuwa 52 kati ya hao watatu hawakurejesha fomu na mmoja kujiudhuru.
Wa tano mstari wa mbele kutoka kulia ni Lameck Airo akiwa kwenye picha ya pamoja na Watia nia Ubunge Jimbo  la Rorya
Watia nia wakiwa kwenye kikao cha maelekezo kutoka kamati ya Siasa wilayani humo ukumbi wa CCM uliopo Utegi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527