TAMWA YAFURAHISHWA UTHUBUTU WA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI UCHAGUZI MKUU 2020 ZANZIBAR
Wakati zoezi la uchukuaji  na urejeshaji fomu kwa nafasi ya Urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likifikia tamati, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar kimefurahishwa na uthubutu wa wanawake kujitokeza kuwania nafasi hizo.

Tamwa Zanzibar imewapongeza kwa dhati wanawake wote waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa wagombea wa kiti cha Urais Zanzibar kupitia chama hicho.

Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya mgombea Urais Zanzibar ulioanza Juni 15, mwaka huu, jumla ya wanachama 32 wamejitokeza kwenye kinyanganyiro hicho ambapo wanachama watano (5) sawa na asilimia 15 walikuwa ni wanawake.

Wanawake hao ni pamoja na Mwantum Mussa, Hassna Attai, Fatma Kombo, Mgeni Hassan na Maudline Castico.

Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 1, 2020 na Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambapo amekipongeza CCM kwa kuwawezesha wanawake hao kuweza kugombea hadi katika hatua hiyo ya uongozi.

"Tunaamimi sasa wakati umefika kwa jamii wakiwemo wanasiasa kulichukulia suala hili kwa uzito unaostahiki na hivyo kuwapa nafasi wanawake kuonesha uwezo wao wa kuongoza katika nyanja mbali mbali.

Tunatamani pia CCM itachagua mmoja kati ya wanawake hao ili kuweza kupeperusha bendera ya Chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020," amesema

Dkt. Mzuri amesema TAMWA Zanzibar inaamini kwamba ujasiri huo ulioonyeshwa na wanawake hao waliojitokeza utasaidia kuongeza hamasa zaidi kwa   wanawake vijana kuendelea kujiamini na kuona kuwa wanayo nafasi sawa ya kushiriki katika ngazi zote za maamuzi kwa mstakabali wa taifa lao.

"TAMWA Zanzibar inawaomba wanawake wa vyama vyengine vyote kujitokeza katika kugombea nafasi mbali mbali ili kuongeza mabadiliko haya ya wanawake katika ngazi za maamuzi itakayopelekea pia kutatuka kwa matatizo mbali mbali yanayowaaathiri kiuchumi na kijamii," amesema.

Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kujitokeza wanawake kugombea katika nafasi hiyo ya juu ya nchi kutokana na mifumo dume ambayo inamtenga mwanamke katika kuwania nafasi za maamuzi sambamba na mwenziwe mwanamme.

Hadi miaka ya 1940 ilionesha kuwa mwanamke alikatazwa kuhudhuria hata skuli, nyenzo muhimu katika kukwaa ngazi za kisiasa na kijamii kwa madai kuwa anaweza kupoteza ujanajike wake.

Hali hii ilirejesha nyuma sana maendeleo ya wanawake na nchi kwa jumla kwa vile wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya wakaazi wa Zanzibar kwa mujibu wa Sensa ya 2012 na makisio ya idadi ya watu yaliyofuata.

Tafiti duniani kote ikiwemo na Zanzibar zinaonesha kuwa wanawake ni watendaji wazuri, waaminifu, waadilifu na wanaofanya maamuzi kwa njia ya ushirikishi na hivyo wakiwa kwenye uongozi huharakisha sana maendeleo ya nchi.


Ni Amina Salim Ali tu ndiye aliyewahi kuomba ridhaa ya wananchi kupitia chama hicho kikuu nchini mwaka 2000 ambapo hakuweza hata hivyo kuchaguliwa na hivyo Zanzibar kukosa kabisa mgombea mwanamke pamoja na Rais mwanamke kwa maisha yote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post