TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA

KUPATIKANA NA SILAHA [GOBOLE] BILA KIBALI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia AMANI MPINDULE [68] Mkazi wa Lualaje kwa tuhuma za kumiliki silaha bunduki aina ya Gobole bila kuwa na kibali.


Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 25.07.2020 majira ya saa 15:00 Alasiri huko katika Hifadhi ya Mwenje – Ruaha iliyopo Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya katika msako wa pamoja kati ya Jeshi la Polisi na Askari wa TANAPA.

Mtuhumiwa alikutwa akiwa na:-
 1. Silaha [Gobole] isiyo kuwa na namba za usajili iliyotengenezwa kienyeji ambayo anaitumia kwa shughuli za uwindaji haramu,
 2.  Goroli tano [05],
 3.  Vipande vinne [04] vya nondo ambavyo hutumika kama risasi na
 4.   Unga wa baruti.
Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

KUKAMATA SILAHA BASTOLA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kukamata silaha bastola yenye namba ya usajili TGT.10582 / PT.809E aina ya TAURUS ikiwa na risasi moja ndani ya magazine iliyotengenezwa nchini Brazil.

Silaha hiyo ilikamatwa mnamo tarehe 25.07.2020 majira ya saa 19:30 Usiku huko Mtaa wa Maendeleo nyuma ya ofisi ya serikali ya Mtaa wa Iyela, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na kubaini mmiliki halali wa silaha hiyo.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA WIZI KWA NJIA YA MTANDAO.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewatia kumtia mbaroni watuhumiwa wanne 1. ISSA SAID [28] Mkazi wa Ilemi 2. JONATHANI FIKIRI TANGANYIKA [23] Mkazi wa Mwambenja 3. OBEDY MWASELELE [24] Mkazi wa Mwamfupe na 4. WILLIAM SALVATORY JONAS @ CHINA TZ [20] Mkazi wa Igoma “B” Jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa njia ya mtandao.

Awali mnamo tarehe 24.07.2020 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipokea taarifa za siri toka kwa moja ya kampuni ya simu kuwa baadhi ya watumishi wake waliopo mkoani Mbeya ambao ni “Freelancer” wanaosajili laini za simu kwa mfumo wa kisasa kwa kutumia “Biometric Machine” kuwa wamekiuka taratibu za usajili wa laini za simu kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania [TCRA].

Kufuatia taarifa hizo, ni kwamba mnamo tarehe 27.07.2020 majira ya saa 17:30 Jioni Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako katika maeneo ya Igodima, Iganzo, Ilemi na Isanga Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wanne na katika upekuzi uliofanyika walikutwa na vitu vifuatavyo:-

 1.     Biometric Machine Moja.
 2.     Simu Smartphone aina ya TECNO Camon inayotumika kusajilia laini.
 3.     Simu mbili Smartphone aina ya TECNO zinazotumika kufanya utapeli.
 4.     Laini 06 za Halotel.
 5.     Laini 11 za Vodacom.
 6.     Laini 01 ya Airtel.
 7.     Laini 48 za Airtel ambazo hazijatumika.
 8.     Laini 02 za Tigo.
 9.     Laini 02 za Zantel.
 10.     ICC ID Card 33 za Halotel.
 11.     ICC ID Card 46 za Vodacom.
 12.     ICC ID Card 17 za Tigo.
 13.     Daftari 02 zenye namba za NIDA za watu mbalimbali ambazo hutumika kufanya uhalifu wa kimtandao.
Watuhumiwa wamekiri kuwa baadhi ya laini huzitumia kufanya utapeli na uhalifu wa kimtandao kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno [SMS] kuhitaji kutumiwa pesa kwenye mitandao mingine “ILE PESA TUMA KWENYE NAMBA HII, JINA LITAKUJA…….”

Aidha watuhumiwa wamekiri kuuza laini hizo ambazo wamesajili kwa majina ya watu wengine kwa bei ya Shilingi 2,000/= kwa kila laini. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

WITO WA KAMANDA.
Ninatoa wito kwa wananchi kuwa makini pindi wanapofanya usajili wa laini zao za simu ili kuepuka kadi zao kutumika kusajili laini za watu wengine. Pia Jeshi la Polisi linasisitiza wananchi kuendelea kuhakiki usajili wa laini zao kwa kubonyeza *106#, kisha chagua namba 2, ingiza namba ya kitambulisho chako cha NIDA kisha utapata ujumbe utakaoonyesha orodha ya namba za simu zilizosajiliwa kwa kitambulisho chako.

Aidha natoa rai kwa makampuni ya simu kuajiri mawakala waaminifu ili kuepuka kuwasajilia watu laini kwa namba za vitambulisho visivyo kuwa vyao na kusababisha kuongezeka kwa wahalifu wa kimtandao na matapeli. Sambamba na hilo ninatoa wito kwa mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kielektroniki hasa simu za mkononi ili kuepuka utapeli na uhalifu wa kimtandao.

Pia ninawataka vijana kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu ambavyo vitawasababisha kupata adhabu kali kwa mujibu wa sheria na kupoteza dira ya maisha yao.

Sambamba na hilo, nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote na Watanzania kwa ujumla sikukuu njema ya EID AL-HAJI. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama katika maeneo yote. Aidha wananchi wanakumbushwa kuzingatia usalama wao kwanza katika makazi yao, katika matumizi ya barabara na katika swala ya EID AL-HAJI itakayofanyika katika Misikiti mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post