SIRI YASIN ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UBUNGE SHINYANGA MJINI KUPITIA ACT WAZALENDO.... ATAKA WANAUME WARUHUSU WAKE ZAO KUGOMBEA UCHAGUZI MKUU 2020

Bi. Siri Yasini Swedi
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo mkoa wa Shinyanga, Mhe. Siri Yasin amewataka wanaume wawaruhusu wake zao kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi Mkuu Tanzania mwaka 2020 huku akiwataka wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kuacha uoga,wajiamini na kuwapuuza wanaowabeza. 

Akizungumza na Malunde 1 blog leo Jumatatu Julai 13,2020 Siri Yasin ambaye tayari amechukua fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini amesema wanawake wanaweza kuwa viongozi hivyo ni vyema jamii ikawapa nafasi ya kuwania nafasi za uongozi. 

“Wanaume wawaaachie wake zao wagombee katika uchaguzi Mkuu, wasiwakatishe tamaa na waachane na mila potofu kuwa wanawake hawatakiwi kuwa viongozi na kuwa na hofu kuwa mwanamke akiwa kiongozi kwamba atashindwa kutekeleza majukumu ya familia”,amesema Siri Yasin ambaye ametumikia uongozi katika Chama Cha Demokrasia na Maendeleo mkoani Shinyanga kwa kipindi cha miaka 17 na sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo mkoa wa Shinyanga tangu mwaka 2015.

“Mimi tayari nimechukua fomu ya kuomba kugombea ubunge jimbo tangu tarehe 11.07.2020 nitarudisha tarehe 20.07.2020 na ninashukuru kuona wanawake wanaendelea kujitokeza kuchukua fomu kuwania ubunge na udiwani mfano hapa Shinyanga wanawake wamejitokeza kuchukua fomu katika kata ya Chamaguha,Ndembezi na Ibinzamata . Naomba wajitokeze zaidi katika maeneo mengine”, amesema Siri Yasin.

Siri Yasini amesema  hivi sasa hali inaridhisha kwani wanaume sasa wanawafurahia wanawake wachapakazi na wanaojiamini ndiyo maana yeye amekuwa kiongozi Mwanamke na wanaume na wanawake wanapenda utendaji kazi wake.

“Kutokujiamini kuna mambo mengi ikiwemo kuwaza kuwa mimi nikienda nani ataniunga mkono ‘nani atani sapoti’ sina hela mkononi,nitasimamaje jukwaani na mambo mengine mengi ambayo yanamsababisha hata hamu ya kugombea inafifia.Hutakiwi kuwaza hayo unachotakiwa kuwaza ni kuona unaweza kufanya nini kwa sababu unajiamini”,amesema. 

Anasema mila na desturi za kwamba mwanamke hawezi kuongoza zimepitwa na wakati kwani sasa jamii ina uelewa na wanawake viongozi wanapewa heshima kama wanavyopewa wanaume na wanawake viongozi wamekuwa na mashabiki wa kike na wa kiume. 

“Uoga ni tatizo kubwa sana kwa wanawake kutothubutu kugombea nafasi za uongozi. Uoga mwingine unatokana na kubezwa kuanzia ndani ya familia,wanawake wengi wanakatishwa tamaa ndani ya familia zao. 

Hata mme wako anaweza kukubeza lakini ukisimama vizuri huyo atakuwa shabiki wako namba moja na atakusaidia kushawishi na kukutafutia kura kwa wanaume wenzake na jamii kwa ujumla. Hakuna mtu anamuunga mkono mtu muoga, hivyo wanaotaka uongozi wasiwe waoga wajiamini”,amesema Siri Yasini.

Siri Yasini anawaomba wanawake wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu 2020 akieleza kuwa mwanamke anaweza kuwa kiongozi vizuri kabisa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527