RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA KUZIKWA JUMATANO JULAI 29,2020 KIJIJI CHA LUPASO MTWARA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa ataagwa Kitaifa Jumanne Julai 28 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na atazikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara Jumatano, Julai 29, 2020.

“Mwili wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu utaanza kuagwa kuanzia Jumapili, Julai 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru ambapo saa 4.00 asubuhi kanisa Katoliki litaongoza ibada na baada ya ibada waombolezaji wataanza kuaga.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 24, 2020) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam. Ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafamilia na Watanzania waendelee kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake.

Amesema zoezi la kuaga mwili litafanyika kwa muda wa siku tatu ambapo wakazi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na wananchi kutoka maeneo mengine wataanza kuaga kuanzia Jumapili, Julai 26 hadi Jumanne, Julai 28 siku ambayo mwili utaagwa Kitaifa.

Waziri Mkuu amesema kwa siku ya Jumanne, Julai 28, 2020 zoezi la kuaga mwili litanyika kuanzia asubuhi hadi saa 6.00 mchana na ifikapo saa 8.00 mchana mwili utasafirishwa kwenda Masasi kwa kupitia uwanja wa Ndege wa Nachingwea na mazishi yatafanyika Jumatano, Julai 29, 2020.

Mapema, Waziri Mkuu alikwenda nyumbani kwa aliyekuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa Masaki jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa Mama Anna Mkapa mjane wa marehemu pamoja na familia, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali.

Amesema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali tumepokea taarifa za msiba wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais wa Awamu ya Tatu kwa masikitiko makubwa. Nawasihi muendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kama alivyosema Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli.”

Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Akitangaza kifo hicho kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari usiku wa kuamkia leo Rais Dkt. Magufuli kwa masikitiko makubwa alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini William Mkapa amefariki dunia hospitalini jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Rais Dkt. Magufuli amewataka Watanzania wote wawe watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Mhe. Benjamin William Mkapa. “Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia.”

Aliongeza kuwa “ Amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele za haki.”

Mwisho.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post