RAIS MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO KWA NJIA YA SIMU NA RAIS WA MSUMBUJI, FILIPE JASINTO NYUSI


RAIS  Magufuli leo  amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Msumbuji, Filipe Jasinto Nyusi ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji na masuala ya kikanda.

Rais Magufuli amempongeza na kumtakia heri Rais Nyusi na wananchi wote wa Msumbiji kwa Taifa hilo kuadhimisha miaka 45 ya tangu kupata uhuru wake.

Rais Magufuli amemwambia Rais Nyusi kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema na Msumbiji kama ulivyoasisiwa na Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moses Machel wa Msumbiji katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, viongozi hao wamezungumzia maandalizi ya kupokezana kijiti cha uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC atamkabidhi uenyekiti wa SADC, Rais Nyusi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa SADC kwa sasa.

Viongozi hao pia wamezungumzia ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) ambapo wamebadilishana mawazo juu ya namna bora ya kukabiliana na ugonjwa huo, hasa namna Tanzania ilivyofanikiwa kupunguza maambukizi yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527