MZEE GULAM ANG'AA KURA ZA MAONI UDIWANI MJINI...NKULILA,MWENDAPOLE,MARIAM NYANGAKA WATOBOA...VICTOR AKITISHA KULE NGOKOLO


Gulam Hafiz Mukadam

Mariam Nyangaka
Hassan Mwendapole
Victor Mkwizu 'Sangu'


David Nkulila
Na Damian Masyenene & Kadama Malunde - Shinyanga
Leo zoezi la upigaji kura za maoni kwa watia nia wa nafasi za ubunge wa kata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeendelea katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo katika Manispaa ya Shinyanga aliyekuwa Mstahiki Meya wa manispaa ya Shinyanga, Gulam Hafiz Mukadam  ameshida kura za maoni kata ya Mjini.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Julai 25,2020 Gulam alikuwa anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwaMwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu, Nassoro Warioba lakini hali ikawa tofauti na kuibuka kidedea.

Gulam amepata kura 25 kati ya 42, huku Nassoro akiambulia kura 4.

Mshike mshike mwingine ulikuwa  Kata ya Ndembezi ambapo aliyekuwa Diwani David Nkulila ameshinda kwa 54 dhidi ya 33 za Victor Thobias Manywa, huku Winsslaus Maganga akiambulia kura moja na Robert Mwelo akikosa kura, ambapo wapiga kura walikuwa ni 88.

Kwa upande wa Kata ya Kitangili Mariam Nyangaka ameongoza kwa kupata kura 44 kati ya kura 79 zilizopigwa, akifuatiwa na Madeha Hamis kura 17 na  Timoth Ngasa kura 16. 

Katika Kata ya Ngokolo ambayo CCM wanahitaji kuirejesha kutoka mikononi mwa upinzani CHADEMA wapiga kura walikuwa 74, ambapo Victor Mkwizu ameibuka mshindi kwa kupata kura 19.

Hata hivyo, Mkwizu alipata ushindani mkubwa akibebwa na kura moja tu mbele ya mpinzani wake, Cecilia Shangaluka aliyepata kura 18, huku Fravel Makwaya na Fue Mlindoko wakipata kura 13 kila mmoja.

Kwa upande wa Kata ya Kambarage, aliyekuwa diwani, Hassan Mwendapole ameibuka kidedea akipata ushindi wa kishindo mbele ya washindani wake baada ya kukusanya kura 46 kati ya 79 zilizopigwa, huku mshindani wake wa karibu Emmanuel Kidinya akipata kura 13, Rehema Namanyiro kura 7, Majid Issa kura 7 na Joyce Masunga kura 4.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527