HUYU NDIYO MENDE MKUBWA ZAIDI WA BAHARINI


Kombamwiko au mende huyo wa baharini alipatikana katika mlango bahari wa Sunda

Mwaka huu taarifa za kisayansi zimehusisha mambo tofauti, dunia kukabiliwa na janga la virusi vya corona na wimbi la nzige wanaokula mazao shambani.

Lakini sasa hivi wanasayansi nchini Indonesia wametangaza kwamba wamepata familia ya mdudu mkubwa zaidi katika kina cha chini cha bahari - ambaye wanamueleza kuwa ni kombamwiko mkubwa wa baharini.

Mdudu huyo ni jamii ya isopodi wenye uhusiano wa mbali na kaa na kamba ambao wako tambarare, miili yao ina ugumu mfano wa aina fulani ya chawa - anayeishi chini kabisa ya bahari.

Kombamwiko au mende huyo wa baharini alipatikana katika mlango bahari wa Sunda kati ya visiwa vya Java na Sumatra, kati ya mita 957 na 1,259 chini ya usawa wa bahari.


Kawaida wadudu hao wanapokua, ukubwa wao huwa ni sentimita 33 na wanachukuliwa kwamba ndio wakubwa zaidi. Lakini kuna spishi nyengine ya wadudu hao ambao ukubwa wao kuanzia kichwani hadi kwenye mkia huwa ni sentimita 50.
Nadhari nyengine ni kwamba chini ya bahari, wanyama wawindaji ni kidogo

"Ukubwa wake ni wa juu zaidi," amesema msimamizi wa utafiti huo Conni Margaretha Sidabalok, kutoka Taasisi ya Sayansi ya Indonesia.

Kuna aina saba pekee za spishi ya isopodi ambazo ni kubwa zinazojulikana duniani.

Pia ni mara ya kwanza aina hii ya kombamwiko amepatikana kwenye kina cha chini ya bahari Indonesia - eneo ambalo utafiti kama huu ni nadra sana, timu inayohusika imesema kupitia jarida la ZooKeys.

Ukubwa wa mende huyo
Kulingana na Makumbusho ya Kitaifa ya viumbe asili Uingereza, kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea kwa nini isipodi wa chini kabisa ya bahari ni wakubwa sana.

Moja wapo inasema kuwa wanyama wanaoishi china ya kina cha bahari wanahitajika kuwa na kiwango kikubwa cha oksijeni, kwahiyo miili yao inakuwa mikubwa na miguu mirefu.

Nadhari nyengine ni kwamba chini ya bahari, wanyama wawindaji ni kidogo na hilo linawapa fursa ya kukua na kuwa wakubwa.
Lakini mbali na muonekano wao wa kuogopesha, sio hatari kama walivyo kimuonekano

Pia aina hii ya wadudu nyama zao mwilini ni kidogo sana ukilinganisha na jamii ya kaa, hivyobasi kutopendelewa na wanyama wawindaji.

Aina hii ya wadudu pia ina pembe ndefu na macho makubwa - na vyote hivyo vinasaidia katika mazingira ya makazi yao ambayo ni giza.

Lakini mbali na muonekano wao wa kuogopesha, sio hatari kama walivyokimuonekano.

Na kawaida wadudu hao huwa ni wawindaji chini ya bahari wanaotafuta wanyama waliokufa kama chakula chao.

Kulingana na Makumbusho ya Taifa ya viumbe asili Uingereza, umeng'enyaji wao wa chakula ni wa pole pole sana, inasemenaka kwamba mdudu jamii ya isipodi aliyekuwa ameshikiliwa Japani aliishi kwa miaka mitano bila kula chochote.
Kombamwiko hao hula wanyama waliokufa chini ya bahari

Katika kipindi cha maonesho ya wiki mbili 2018, timu hiyo iligundua na kukusanya maelfu ya wadudu kutoka maeneo 63 tofauti tofauti ya utafiti na kubaini spishi mpya.

Timu inaelezea spishi hiyo ilikuwa ni mume mmoja na jike mmoja wenye ukubwa wa sentimita 36.3 na 29.8 mtawalia.

Pia spishi nne za wadudu hao wadogo zilichukuliwa kutoka kwenye maji ya mlango bahari wa Sunda na kusini mwa Java, lakini Sidabalok amesema hawakuweza kuwabaini ni spishi gani kwasababu baadhi ya viungo vyao vilikuwa bado havijajitokeza.

Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527